Wawekezaji wazawa wahimizwa uzalendo

WATANZANIA wanaofanya uwekezaji kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya na elimu wamehimizwa kulipa kipaumbele suala la uzalendo ili miradi yao isiwe kibiashara tu bali pia iwe sehemu ya huduma za kijamii.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025, Ismail Ali Ussi amehimiza hayo akiwa wilayani Mbogwe mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Kituo cha Afya binafsi cha Gakala.

Ussi amesema serkali ya awamu ya sita imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wote huku kipaumbele kikiwa ni kwa wazawa jambo ambalo ni fursa inayopaswa kutumika kwa ufasaha kuchagiza maendeleo.

SOMA: Mwenge wa Uhuru wawasili Geita

Amesema uwekezaji wenye tija ni ule unaoambatana na uzalendo hususani kwa kulipa kodi na kutoa ajira bila upendeleo na kipaumbele kikiwa kwa vijana wa kitanzania ili kuisaidia serikali kukatibili ukata wa ajira.

Ussi ametaja kituo cha afya Gakala kuwa ni miongoni mwa uwekezaji wa mfano kwani mmiliki ametoa fursa kubwa ya ajira kwa vijana wa kitanzania ambao wamebobea kwenye fani na taaluma mbalimbali.

“Leo hii vijana wetu waliosomea fani za udaktari uhudumu, kukaribisha wageni, fani za usafi, wamepata ajira katika eneo hili, na hakuna mtu anayetoka nje ya Tanzania ambaye ameajiriwa katika hospitali hii.” amesema.

Amesema wawekezaji wote pia wanalo jukumu la kuunga mkono kampeni ya serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuwezesha ufanisi wa kupiga vita matumizi ya kuni na mkaa na kusaidia kulinda mazingira.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Afya Gakala katika kata ya Bukandwe, Bunga Dadu amesema mradi una thamani ya sh bilioni tatu na mpaka sasa sh milioni 539 zimetumika kwa awamu ya kwanza.

Amesema mradi ulianza kutekelezwa Desemba 18, 2024 kwa hatua ya kwanza ya ujenzi wa jengo la OPD, Jengo la RCH, Jengo la Utawala, Jengo la Upasuaji, kichomea taka, shimo la kutupia kondo na jiko.

“Lengo la mradi ni kusaidia kusaidia wananchi wa kata ya Bukandwe na kata jirani kupata huduma bora za afya na kibingwa. Vilevile mradi huu utasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto”, amesema Dadu.

Naye Mkuu wa wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed amesema mpaka sasa wilaya ina vituo vya afya saba vinavyotoa huduma na kukamilika kwa kituo cha Afya Gakala kitaongeza kufika vituo nane.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button