Wazabuni kujengewa uwezo malalamiko, rufaa NeST

ARUSHA: MAMLAKA ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewasihi wazabuni kushiriki mafunzo yanayoratibiwa na mamlaka hiyo ili kuwajengea uwezo wa kutumia moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST.
Hatua hiyo ni katika jitihada za kuhakikisha serikali inapata thamani halisi ya fedha katika miradi yake.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando pembezoni mwa Kongamano la 9 la Ununuzi wa Umma la Mwaka 2025 linaloendelea Arusha.
Amesema moduli imejengwa ili kusaidia umma na hususan kuendana na miongozo ya serikali ya kuzitaka taasisi za umma kutumia tehama katika kufikisha huduma zake kwa wananchi kwa wakati uliokusudiwa.
Baada ya serikali kupitia Wizara ya Fedha kuzindua rasmi matumizi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST,Februari 2025, PPRA imeendeleza zoezi la kutoa mafunzo mahususi ya matumizi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kieletroniki katika Kanda mbalimbali nchini.
“Katika kuhakikisha wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma wanapata mafunzo ya matumizi ya moduli PPAA imeendelea na zoezi la kutoa mafunzo mahususi ya Moduli katika kanda mbalimbali ambapo hadi sasa Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zimepatiwa mafunzo hayo”.