Wazazi, walimu watakiwa kutoa ushirikiano kwa watoto wa kiume

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Boys Initiative Tanzania imeadhimisha Siku ya Mtoto wa Kiume Duniani kwa mafanikio makubwa kwa kuandaa mdahalo wa kielimu uliowakutanisha wanafunzi kutoka shule za msingi Kibondemaji na Kizuiani, zilizopo katika Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Mdahalo huo, ambao umefanyika kwa lengo la kuhamasisha uelewa na kuchochea mabadiliko chanya kwa watoto wa kiume, ulijikita katika mada kuu: “Ukuaji wa Kielimu kwa Mtoto wa Kiume”. Kupitia mjadala huu, changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kiume katika safari yao ya elimu zilijadiliwa kwa kina.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dianarose Rweyemamu, amesema mdahalo huo uliibua masuala nyeti kama vile matokeo yasiyoridhisha ya kitaaluma kwa watoto wa kiume, pamoja na ongezeko la idadi ya wavulana wanaoacha shule kabla ya kuhitimu. Aidha, ameeleza kuwa watoto wa kiume wamekuwa wakipungua kwa kasi katika nafasi za uongozi wa kitaaluma kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi taifa.

SOMA ZAIDI: Watoto wa kiume wawezeshwe pia

“Changamoto hizi zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa morali ya masomo kwa wavulana, kuwafanya waingie mapema katika ajira zisizo rasmi, na hata kuathirika kisaikolojia. Tunapaswa kutambua kuwa mtoto wa kiume anastahili uangalizi na msaada kama ilivyo kwa mtoto wa kike,” amesisitiza Rweyemamu.

Kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Wilaya ya Temeke, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibondemaji ametoa salamu maalumu akisisitiza umuhimu wa kuiadhimisha siku hii kitaifa, akibainisha kuwa ni fursa muhimu ya kutafakari na kuchukua hatua madhubuti kwa ajili ya maendeleo ya watoto wa kiume.

Hafla hiyo pia imeambatana na burudani mbalimbali za kitamaduni na kisanaa ikiwemo ngonjera, mashairi, maigizo, ngoma za asili, utenzi na mdahalo rasmi ulioshirikisha wanafunzi kutoka shule zote mbili.

Boys Initiative Tanzania inaendelea kujitolea kukuza usawa wa kijinsia katika malezi na elimu, kwa kuhakikisha kuwa watoto wa kiume wanapewa nafasi ya kusikilizwa, kuelekezwa na kuendelezwa kama sehemu muhimu ya jamii inayojali haki na maendeleo ya wote.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button