Waziri Mavunde asimamisha uchimbaji madini Mto Zila

Waziri wa Madini, .Anthony Mavunde  amesimamisha shughuli za uchimbaji zilizokuwa zikifanywa na kampuni ya G & I Tech Mining Company Ltd kwa kipindi hiki cha masika na pia mpaka pale tathmini ya kitaalam ya mazingira itapokamilika juu ya shughuli za uchimbaji madini kwenye Mto Zila mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo Waziri Mavunde ameyasema hayo katika kijiji cha Ifumbo, Wilayani Chunya alipotembelea eneo la leseni ya mwekezaji ambalo lilivamiwa na wananchi na kusababisha mgogoro mkubwa na uharibifu wa mali za mwekezaji huyo.
“Tumetembelea maeneo yote mawili, na sote tumejionea hali halisi ya mazingira. Ni dhamira na maelekezo ya Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan kuona shughuli zote za kiuchumi hususan za madini zinafanyika kwa utulivu bila kuleta migogoro na pasipo kuathiri mazingira ya eneo shughuli zinapofanyika.
Amesema amesikiliza hoja za wananchi juu ya uharibifu wa mazingira ya Mto Zila na kwamba Serikali itaunda Timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina ya mazingira juu ya athari zinazoweza kutokea wakati wa uchimbaji wa madini na kwasasa shughuli zote za uchimbaji madini zisimame kipindi hichi cha masika kama NEMC ilivyoelekeza.
Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Watalaam wa Mazingira, wataalam wa Mkoa na wananchi katika muda mfupi ujao inakwenda kuunda timu ya pamoja ya kufanya tathmini ili kueleza kitaalam iwapo shughuli hizo zinaweza kuendelea kufanyika pasipo athari kwenye mazingira ya Mto Zila.
“Nitumie fursa hii kuwataka wananchi wote kuacha vitendo vya uvunjifu wa amani na kujichukulia sheria mkononi, tunalaani kitendo cha kuvamia na kuharibu mali za mwekezaji,“amesema Mavunde.
Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga ameshukuru ujio wa Waziri wa Madini na kusisitiza kwamba sasa anaona mwanga ambao unakwenda kuleta suluhisho la kudumu.