Waziri Mkuu atangaza kuomba tena ridhaa Ruangwa

DODOMA — Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza rasmi nia yake ya kugombea tena ubunge wa Ruangwa katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 2025, akieleza imani yake kwa wananchi waliompa ushirikiano kwa miaka yote.
Akiwashukuru wakazi wa Ruangwa, alisema licha ya majukumu yake kitaifa, wameendelea kuwa nguzo yake ya kisiasa na kiutu, na kwamba atarudi nyumbani kuchukua fomu ya kugombea kwa heshima.
“Ninakuja kuchukua fomu ya kuomba ridhaa yenu tena,” alisema Majaliwa kwa hisia, akisisitiza kuwa mapenzi ya wananchi yamempa nguvu ya kutumikia taifa.
Pia alimshukuru mke wake na familia yake kwa uvumilivu, hasa alipokuwa nje ya jimbo na nyumbani kwa shughuli za kitaifa. Alisema mshikamano wao umekuwa msaada mkubwa kwake.
Majaliwa alitumia nafasi hiyo kuwatakia kila la heri viongozi wengine wanaojiandaa kugombea majimbo yao akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika uchaguzi ujao.