WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezipongeza klabu za Simba na Yanga kwa kutuwakilisha vizuri katika mashindano ya vilabu barani Afrika.
“Nianze kwa kuipongeza Timu ya Simba kwa kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika na kuchuana na miamba ya soka barani Afrika. Ninawapongeza sana kwa kufanikiwa kufika hatua ya Robo Fainali ambapo ilipambana na Timu ya Wydad Cassablanca ya Morocco.” Amesema Majaliwa.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo wakati kuwasilisha hotuba yake mbele ya Bunge, Waziri Majaliwa ameipongeza pia Yanga kwa heshima kubwa waliyoiletea nchini kwa kufanikiwa kwa mara ya kwanza kucheza fainali katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
“Sote tunatambua timu ya Yanga haikutwaa ubingwa kutokana na USM Alger kupata magoli mawili ya ugenini, kitendo kilichopelekea Yanga kushika nafasi ya pili na kutunukiwa medali za fedha. Nami niungane na Watanzania kuwapongeza Wanayanga kwa hatua hiyo muhimu.” Amesema Waziri Majaliwa.
Katika hotuba hiyo Waziri Mkuu, Majaliwa aliitaja klabu ya Yanga mara sita na watani wao Simba mara mbili.
Comments are closed.