Waziri Mkuu: Vijana msiogope kukopa mitaji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wasiogope kukopa ili kupata fedha za mitaji ya kibiashara lakini pia akawasisitiza wawe tayari kurejesha mikopo hiyo.

“Vijana wetu msiogope kukopa ili kupata mitaji. Bila kukopa huwezi kupata maendeleo. Eneo muhimu ni kupata taasisi za fedha kama CRDB lakini kikubwa zaidi ni kuwa tayari kulipa. Dawa ya kukopa ni kulipa,” amesema.

Ametoa wito huo leo mchana Jumapili, Machi 12, 2023, wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria semina ya uwekezaji na ufunguzi rasmi wa dirisha la kupokea maombi ya ushiriki wa programu ya iMBEJU ya Benki ya CRDB uliofanyika kwenye ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam.

iMBEJU ni programu maalumu ya CRDB ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake wajasiriamali ambayo ilizinduliwa Oktoba, 2022 katika Kongamano la Sita la TEHAMA lililofanyika Zanzibar.

Waziri Mkuu amewataka vijana na wanawake wajasiriamali watakaoshiriki programu hiyo waitumie fursa hiyo ipasavyo hasa ikizingatiwa kuwa watawezeshwa kupata elimu ya biashara, stadi za biashara na pia watawezeshwa kimitaji.

Benki ya CRDB imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Kamisheni ya Tehama (ICT-C) na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika kuinua vipaji kwenye masuala ya sayansi na teknolojia.

“Wizara ya Ujenzi waone njia ya kuwawezesha vijana hawa ili waanze pilot project pale kwenye taa za UWT, FIRE na Muhimbili. Na kama siyo hapo, watafutiwe barabara nyingine yenye msongamano ili waweke mfumo wao na waoneshe ubunifu wao na pia sisi tupate suluhisho,” amesema.

Amesema Serikali imeendelea kutumia mifuko ya kukopesha vijana ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na mitaji iliyokuwa ikikwamishwa na uwepo wa masharti magumu kutoka kwa taasisi za fedha ikiwemo mabenki.

“Kwa mfano, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.88 imetolewa kwa miradi 85 ya vijana.”

Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema Serikali inatarajia kwamba programu ya iMBEJU itazalisha teknolojia mahsusi kwa ajili ya Watanzania.

Habari Zifananazo

Back to top button