Wema Sepetu aomba radhi kwa watanzania

DAR-ES-SALAAM : MSANII maarufu wa filamu nchini na Mkurugenzi wa Taasisi ya Wema wa Mama, Wema Sepetu, ameomba radhi kwa kuvaa mavazi yaliyozua mjadala kuhusu maadili na kuahidi kuwa tukio hilo halitarudiwa tena.
Wema, anayefahamika pia kama Tanzania Sweetheart, alitoa msamaha huo baada ya kuitikia wito wa Bodi ya Filamu Tanzania kufuatia picha zake zilizosambaa mitandaoni na kuzua mijadala mikali kuhusu maadili ya wasanii.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Wema alisema kilikuwa si kikao rasmi cha kisheria bali ni cha mazungumzo ya kukumbushana kuhusu maadili ya wasanii nchini.
“Nilikuja Bodi ya Filamu kuitikia wito. Kikao hakikuwa rasmi, bali kilikuwa cha kukumbushana juu ya maadili. Nimeyasikia na nimeyazingatia,” alisema kwa unyenyekevu.
Msanii huyo alikiri kuwa alikosea, lakini akaeleza kuwa amejifunza kutokana na tukio hilo na sasa anatambua vyema nafasi yake kama mtu mwenye ushawishi mkubwa katika jamii.
“Kufanya kosa si kosa, bali kurudia kosa ndio kosa. Nachukua nafasi hii kuomba msamaha kwa wote niliowakwaza. Nimejifunza, na haitajirudia tena,” alisisitiza Wema.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaomba radhi mashabiki wake na wale wanaomchukulia kama kioo cha jamii, akiwahakikishia kuwa atakuwa makini zaidi na mienendo yake.
“Niwashukuru Bodi ya Filamu kwa upendo wao. Nimejifunza kuwa nafasi yangu ni kubwa sana katika jamii. Naomba msamaha kwa wote niliowakwaza,” aliongeza.
SOMA: Bodi ya filamu yamwita Wema Sepetu
Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya wasanii katika kulinda maadili, huku wadau mbalimbali wakihimiza umuhimu wa kuwajibika kijamii kutokana na ushawishi walionao.



