Wizara ya Afya yajipanga kuhudumia washiriki mkutano wa Nishati Afrika

WIZARA ya Afya imesema imechukua tahadhari zote zinazohusu masuala ya afya kwa ajili ya kuhudumia viongozi na wageni watakaohudhuria Mkutano Mkuu wa Nishati Afrika unaoanza leo Dar es salaam.
Mkutano huo utakaofanyika kwa siku mbili mfululizo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), unawakutanisha wakuu wa nchi za Afrika, mawaziri wa fedha na nishati, wakuu wa taasisi za kimataifa na washiriki zaidi ya 2,600 wa ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza jana kwenye Hospitali ya Agha Khan ikiwa ni ziara ya ukaguzi wa hospitali mbalimbali zilizoandaliwa kwa ajili ya kuhu[1]dumia wageni hao, Waziri wa Afya, Jenister Mhagama alisema nchi kupitia wizara hiyo imejiandaa vizuri kuhudumia washiriki watakaopata dharura kiafya.
“Ili kuufanya mkutano huu uendelee kuwa salama ni kuzitayarisha taasisi zetu ambazo zimebobea kwenye utoaji wa tiba za kibingwa na kibobezi kuanza kujiandaa na kuchukua tahadhari ya kutoa matibabu ya namna yoyote na kwa jambo lolote litakalotokea katika kipindi hiki cha mkutano,” alisema Mhagama.
Aliongeza: “Kama waziri mwenye dhamana ya Afya pamoja na maandalizi ya muda mrefu leo nimekagua eneo la dharura katika hospitali hii ili kuangalia kama kila kinachotakiwa kuwepo kipo, nimeangalia eneo la wagonjwa mahututi (ICU) mahali viongozi au wageni watataka huduma za kimataifa, eneo la vifaa tiba vifaa vya kiuchunguzi kwa kweli niseme taasisi hii iko tayari hivyo tumejiandaa na kuchukua tahadhari ya kutoa matibabu ya aina yoyote.”
Mhagama alisema serikali itautumia mkutano huo kutangaza utalii wa tiba. Mganga Mkuu wa Taasisi ya Afya ya Agha Khan, Dk Harrison Chuwa alisema hospitali yao imejiandaa kwa ajili ya kutoa huduma nzuri washiriki wa mkutano huo ili kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa



