Wizara ya Afya yapigwa jeki vita dhidi ya malaria

DAR ES SALAAM; WIZARA ya Afya nchini imepokea msaada wa vifaa vya maabara hadubini ‘Microscope’ 133 kutoka kwa Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI).
Akizungumza leo Novemba 14, 2023 Mkurugenzi wa Ofisi ya Afya kutoka USAID Tanzania, Anne Murphy amesema kuwa hadubini hizo 133 zitasambazwa katika vyuo vya kati vinavyosimamiwa na Wizara ya Afya pamoja na Taasisi za Tafiti.
Amesema lengo ni kusaidia kuimarisha uwezo wa wataalamu wa maabara nchini katika upimaji wa vimelea vya malaria kwa ufanisi.
Vifaa hivyo vina thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 448,000 sawa na Sh bilioni 1.2 ambapo vitasambazwa katika vyuo vya kati ambavyo vipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Tanga, Mara na Singida, ili kusaidia upimaji wa vimelea vya Malaria na magonjwa mengine kwa ufanisi zaidi ikiwa ni mpango wa kupambana na ugonjwa huo.
Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS) kimekabidhiwa hadubini 12 kwa niaba ya vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Afya vinavyotoa mafunzo ya kozi ya maabara vilivyopo katika mikoa hiyo sita.

Amesema kuwa hadubini hizo na vitendanishi vingine vya maabara vilivyotolewa vitawezesha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kuimariasha uwezo wa kimaabara katika uchunguzi na kusaidia utoaji matibabu ipasavyo hivyo kusaidia kuokoa maisha ya watu na kuzuia madhara ya malaria.
Ameipongeza Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa za kupambana na kuhakikisha kiwango cha malaria kinashuka nchini kutoka asilimia 14 mwaka 2015 mpaka asilimia 8 mwaka 2022.
Awali akitoa salamu za ufunguzi , Mkurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili Profesa Mohamed Janabi ameishukuru Marekani kwa msaada huo uliolenga kusaidia kuendelea kupambana na kuutokomeza ugonjwa wa malaria nchini.`
“Malaria ni tatizo kubwa linauwa watu 500,000 kila mwaka na bahati mbaya asilimia 96 ya vifo hivyo vinatokea Afrika, takwimu za mwaka jana kila baada ya dakika mbili kuna mtoto mmoja Afrika anafariki kwa ajili ya malaria,”amesema Janabi na kuongeza

“Ni tatizo kubwa, hivyo vifaa hivi vitatusaidia kwa wanafunzi wetu hapa kusoma kwa kina na wakitoka hapa wanakua wabobezi na ndio watakuwa wataalamu wa afya katika vituo vya afya, naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhimarisha uhusiano na mataifa ya nje ambao leo wametuletea msaada huu mkubwa.
Amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kipindi ambacho serikali kupitia Wizara ya Afya imewekeza fedha nyingi ili kuboresha huduma za afya nchini kwa kununua dawa na vifaa tiba.



