Yametimia baada ya miaka 22 fidia Mtwara

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA), imewakabidhi fedha ya fidia wananchi wapatao 50, waliokuwa wanaidai mamlaka hiyo kutokana na eneo ambalo serikali ilichukuwa miaka 22 iliyopita, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji.
Wananchi hao walikabidhiwa fedha hizo Jumatano na kutakiwa kuondoka eneo la Mangamba Juu Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara ndani ya siku 90.
Eneo hilo lilichukuliwa karibu miaka 22 iliyopita na MTUWASA, kwa ajili ya ujenzi wa chujio la maji, lakini wananchi waligoma kuondoka wakidai fidia ya eneo bila mafanikio.
Mapema mwezi huu Rais Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi milioni 816.78, kwa ajili ya kuwalipa wananchi hao, ambapo kwa sasa wamekabidhiwa fedha hizo na kutakiwa kuondoka kupisha utekelezaji wa mradi huo wa Maji.
Maofisa wa mazingira kutoka Wizara ya Maji walifika mkoani hapa na kusimamia na kuhakiki ulipaji wa fidia hiyo kwa wananchi.
“Tunatoa rai kwa wananchi wote ambao wamepata fidia ,tunaomba wasifanye uharibifu wowote wa mazingira, waondoke kwa utaratibu kwa sababu mimea na ardhi ile imeshalipwa,” amesema Ofisa Mazingira kutoka Wizara ya Maji, Moses Mgala.
Kwa upande wake Mkurungenzi Mtendaji wa MTUWASA, Mhandisi Rejea Ng’ondya, ameshukuru serikali kwa kulipa fidia hiyo, huku akiwapongeza wananchi hao pamoja na serikali ya kijiji kuwa wavumilivu kwa miaka 22 kusubiria fidia.