Yanga Geita watoa ‘Azimio’ sakata dabi ya Kariakoo

UMOJA wa Matawi 12 ya wanachama wa Klabu ya Yanga mkoani Geita wameunga mkono uamuzi wa viongozi wao kutocheza mchezo mwingine wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Maazimio ya wanachama hao yametolewa mbele ya waandishi wa habari baada ya kuitisha mkutano wa dharura mjini Geita na kusisitiza kwa kauli moja kuwa wanataka kuona haki inatendeka.

Advertisement

Mratibu wa Matawi ya Yanga Mkoa wa Geita, Rajab Mohamed akisoma maazimio ya wanachama wa Yanga Geita amesema uamuzi uliotolewa na Rais na Makamu wa Rais wa Yanga ni sahihi.

“Wanachama na mashabiki wa Yanga ndani ya mkoa wa Geita, tunaungana na viongozi wetu wa makao makuu, hatuhitaji busara kutatua mgogoro huu unaoendelea.

“Tunaamini bodi ya ligi inaongozwa na sheria pamoja na kanuni zake, basi viongozi wa bodi ya ligi kutatua huu mzozo na siyo watuambie masuala ya busara na hekima. Kama Yanga amevunja sheria ama Simba amevunja sheria, basi TFF na bodi ya ligi wakae chini wapite hizo sheria,” amesema Rajabu.

Ameongeza, pia wanachama wa Yanga mkoani Geita hawana imani tena na uongozi wa bodi ya ligi na wanamtaka Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuacha kutoa kauli za kebehi na uchochezi.

Ofisa Mhamasishaji wa Matawi ya Geita (Yanga Dhahabu), Ahmed Suleyman amesema kilichofanya wakose imani na bodi ya ligi ni kutokana na mfululizo wa matukio yanayominya haki za klabu ya Yanga.

“Kuna makosa ya kibinadamu ambayo watani zetu Simba wamekuwa wakinufaika nayo, kwenye ligi na tulikuwa tunachukulia kawaida lakini kwa hiki kiichotokea inaonyesha kuna maelekezo yapo nyum yake,” amesema.

Msemaji wa Yanga mkoa wa Geita, Deogratius Steven amesema uamuzi wao unalenga kupigania maslahi ya mashabiki wa soka nchini kwani watu walipata hasara kubwa baada ya dabi ya kariakoo kuahirishwa.

Amesema yeye alipata hasara ya takribani sh laki nane baada ya kusafirisha familia yake kwenda jijini Dar Es Salaam kushuhudia dabi ya Kariakoo lakini mchezo ukaahirishwa.

Mjumbe wa Mkutano mkuu wa klabu ya Yanga taifa tawi la Bwanga, Mathayo Athuman amesema viongozi wa mpira waliopo wanapaswa kusimama kwenye haki na siyo kuongoza kwa maslahi binafsi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *