TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imekamilisha uandikishaji wa wapiga kura wapya katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, linalotarajiwa kuwekwa hadharani hivi karibuni kwa ajili ya uhakiki wa mwisho.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji George Kazzi alisema hayo jana baada ya kukamilisha shughuli za uandikishaji wa wapiga kura wapya katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema baada ya kukamilisha mchakato wa kuandikisha wapiga kura wapya, kazi inayofuata ni kuweka hadharani majina ya wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Jaji Kazzi alisema lengo la kuweka daftari hilo hadharani ni kutoa nafasi kwa wananchi kuhakiki majina yao kama yapo sawa pamoja na kuwezesha uwekaji wa pingamizi kwa watu wasio na sifa au wanaotiliwa mashaka.
Alisema hiyo ni hatua muhimu katika maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu na baada ya hatua hiyo, tume itajiridhisha kuwa wapiga kura wote waliomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni halali.
“Tumekamilisha uandikishaji wa wapiga kura wapya katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ikiwa ni wale waliofikisha umri wa miaka 18 ambao hawajaandikishwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu,” alisema.
Mapema, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina alisema uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Unguja na Pemba umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, sambamba na matarajio yake kufikiwa.
Alisema ingawa ni mapema kutaja takwimu halisi za wapiga kura wapya walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, mwenendo unaonesha wananchi walihamasika kwa kiwango kikubwa kujiandikisha, hatua ambayo itawawezesha kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tume hatuwezi kutoa takwimu halisi ya wapiga kura wapya walioandikishwa kwa sasa, lakini uhamasishaji ulikuwa mkubwa sana,” alisema.
Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, Ayoub Mohamed alisema uandikishaji wa wapiga kura wapya katika daftari hilo umefanyika vizuri, na wenye sifa pekee ndio walioandikishwa.
“Kwa ufupi, sisi wajumbe wa ZEC, ambao katika kipindi cha mwezi mmoja tulikuwa tukifuatilia uandikishaji, tumeridhika kwa kiasi kikubwa na uandikishaji wa wapiga kura wapya, ambao kwa asilimia 90 ni vijana,” alisema.