ZELENSKY: Niko tayari kuwaachilia mateka wa Korea Kaskazini

UKRAINE : RAIS wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, amesema kuwa nchi yake iko tayari kumkabidhi kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliokamatwa.
“Mbali na wanajeshi wa kwanza kutoka Korea Kaskazini waliokamatwa, bila shaka kutakuwa na wengine zaidi. Ni suala la muda tu kabla ya wanajeshi wetu kuweza kuwakamata wengine,” alisema Zelenskiy kupitia mtandao wa X.
Zelensky amesema makabidhiano ya mateka hao wawili yataenda sambamba na kuwaachilia mateka wa Ukraine waliokamatwa na Russia. SOMA: Urusi Ukraine wabadilishana mamia ya wafungwa
Wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini walikamatwa katika mkoa wa Kursk, Russia, na hii ni mara ya kwanza kwa Ukraine kutangaza kushikwa mateka kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wakiwa hai tangu walipojiunga na vita karibu miaka mitatu iliyopita, kati ya msimu wa joto na baridi.
Kwa mujibu wa makadirio ya Ukraine na nchi za Magharibi, wanajeshi 11,000 kutoka Korea Kaskazini walipelekwa katika mkoa wa Kursk ili kuwasaidia wanajeshi wa Russia. Hata hivyo, Russia haijathibitisha wala kukana taarifa kuhusu kukamatwa kwa wanajeshi hao wa Korea Kaskazini.



