Masoko ya nyama nje yaongezeka

BODI ya Nyama Tanzania (TMB), imesema masoko ya nyama nje ya nchi yameendelea kuongezeka  kwa kasi huku ikitarajiwa China kuwemo.

Msajili wa Bodi ya Nyama nchini, Dk Daniel Mushi alisema hayo hivi karibuni mjini Morogoro kuwa  hivi sasa Tanzania inauza nyama kwenye nchi za Qatar, Falme za Kiarabu(UAE), Oman, Saudi Arabia, Bahrain, Jordan, Kuwait, Hong Kong, Vietnam, Kenya na Visiwa vya Comoro.

Dk Mushi alisema kwa kipindi cha miezi mitano kuanzia Julai hadi  Novemba mwaka huu, jumla ya tani 4,374 za nyama zenye thamani ya Dola za Marekani 16,760,284 zimesafirishwa kwenda masoko ya nje ya nchi.

Alisema uzalishaji wa nyama nchini umeendelea kuongezeka ambapo katika mwaka 2020/2021 , tani za nyama 738,165 zilizalishwa kupitia viwanda na machinjio mbalimbali  nchini.

Dk Mushi alisema katika mwaka wa 2021/2022 uzalishaji wa nyama uliongezeka kwa asilimia 4.3 ukilinganisha na mwaka wa fedha wa 2020/2021 ambapo jumla ya tani 769,966 zilizalishwa.

“Ongezeko hili kwa kiasi kikubwa limechangiwa na kuendelea kuongezeka kwa viwanda vya nyama na machinjio ya kisasa  na biashara  ya nyama hasa katika soko la nje imeendelea kukuwa kwa kasi,” alisema.

Dk Mushi alisema katika mwaka wa 2020/2021, Tanzania iliuza jumla ya tani 1,774 katika masoko mbalimbali ya kimataifa, na mwaka uliofuata (2021/2022), imeuza tani 10,415, hii  ni sawa na ongezeko la asilimia 487.

Alisema ukuaji huo umechangiwa na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi za kutafuta masoko mapya ya nyama nje ya nchi.

“Uwekezaji kwenye viwanda vya nyama kama wa Nguru Hills Ranch Ltd  umekuwa kichocheo muhimu kwenye ukuaji wa mauzo ya nyama nje ya nchi pamoja na maendeleo ya tasnia ya nyama kwa ujumla,” alisema.

Akizindua  machinjio ya kisasa ya mifugo ya Nguru Hills Ranch Ltd yaliyojengwa wilayani Mvomero mkoani Morogoro, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alimpongeza  Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na uongozi wake mahiri.

Ndaki alisema kutokana na uongozi huo mahiri umeifanya  nchi yetu iendelee kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii  ikiwemo sekta ya mifugo na uvuvi kwa kufunguka  masoko ya nyama ya nje ya nchi.

“Kwa sasa soko limepanuka zaidi kwani tunatarajia kuanza kuuza soko la China na hii  baada ya Rais  Samia kufanya ziara nchini humo na milango imefunguka kwa mazao ya nyama kutoka Tanzania na mojawapo ni samaki na ng’ombe,” alisema.

Waziri Ndaki alizindua machinjio hiyo ambao ni  uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kwa ubia na wanahisa Eclipse Investiment (LLC) kutoka Oman na Kampuni ya Busara Investiment (LLP) ukigharimu dola za Marekani milioni 15 sawa na Sh bilioni 29 yakiwa na  uwezo kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 1,000 kwa siku.

Habari Zifananazo

Back to top button