Wafanyabiashara watakiwa kuzifahamu sheria za ushindani

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara, Sempeho Manongi, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, amewataka wafanyabiashara na wadau wa soko nchini kujielimisha kuhusu sheria za ushindani ili kuepuka changamoto za kisheria zinazoweza kuathiri shughuli zao.

Akizungumza Machi 3, 2026 wakati wa ufunguzi wa semina ya wadau jijini Dar es Salaam, amesema uelewa wa sheria hizo ni msingi wa kulinda maslahi ya washiriki wa soko na kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.

Amebainisha kuwa elimu inayotolewa na Baraza la Ushindani (FCT) inalenga kujenga mazingira bora ya biashara yenye uwazi, usawa na ulinzi wa mlaji, badala ya kutoa adhabu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa FCT, Mhe. Jaji Rose A. Ebrahim, amewahimiza wafanyabiashara kuepuka vitendo vinavyokiuka sheria kama kupanga bei, kugawana masoko au kuingia mikataba inayodhoofisha ushindani.

Amesema biashara inayozingatia uadilifu husaidia kupunguza gharama za maisha na kuongeza ubora wa bidhaa na huduma sokoni.

Ameongeza kuwa Baraza limeimarisha mifumo yake kwa kutumia TEHAMA na kuongeza uwazi katika utoaji wa maamuzi ili kuhakikisha rufaa zinashughulikiwa kwa haraka na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Naye Msajili wa FCT, Wema Mbegu Kaskasi, amesema jukumu la Baraza ni kusikiliza na kuamua rufaa zinazotokana na maamuzi ya mamlaka za udhibiti ikiwemo FCC, EWURA, LATRA, TCAA, TCRA na PURA. Amesema semina hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kutoa elimu kwa wadau, ambapo tayari Baraza limefikia mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanazifahamu na kuzitumia huduma zake kwa urahisi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button