Waipongeza serikali ulinzi rasilimali za misitu

 

MTWARA: WAFANYABIASHARA wa mazao ya misitu Kanda ya Kusini wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuweka mikakati thabiti ya uhifadhi na ulinzi wa rasiliamali za misitu nchini.

Mmoja wa wafanyabiashara wa kiwanda cha utengenezaji wa samani zitokanazo na mazao ya misitu kutoka mkoani Mtwara, Zaidi Hamad amesema wakala huo umekuwa ukifanya vizuri kuchukua  hatua za uthibiti kwa wasio na leseni ambao hijipenyeza kuvuna misitu na usafishaji.

Hamad amesema hayo kuelekea Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti kitaifa itakayofanyika Machi 21 mkoani Lindi.

Licha hayo ametoa wito kuongezwa kwa kasi ya utoaji wa elimu kwa jamii na hamasa ya upandaji wa miti ili kukidhi mahitaji makubwa ya mazao ya misitu hususani ya mbao katika ukanda wa kusini.

“Elimu zaidi inahitajika kwa jamii ili ijitokeze kujenga utamaduni wa kupanda miti kwa lengo la kuzuia uhaba wa rasilimali hizi muhimu hapo baadaye kwa kizazi kijacho,” amesema  Hamad.

Naye, Said Ally mkazi wa Masasi amesema kwa sasa upo umuhimu wa kuoanisha udhitibi wa misitu na kuchukua  jitihada za makusudi za upandaji wa miti mipya hasa ya mbao kutokana na mahitaji makubwa ya wafanyabiashara wa mbao katia ukanda huo.

Kwa upande wake Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Dismass Mrwana ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Leseni Kanda ya Kusini amesema uvunaji wa mazao ya misitu ni biashara halali ambayo ipo kwa mujibu wa sheria na kanuni za misitu.

Amesema Kanda ya Kusini inajumuisha mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma na kuwa biashara hiyo inafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ili kuleta uendelevu au matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Mbali na hayo amesema wadau wanaojisajili ili kufanya biashara mbalimbali za mazao ya misitu na alisema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 waliosajiliwa walikuwa 1,694 .

Mrwana amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuanzia kipindi cha Julai hadi kufikia Machi 13, mwaka huu waliosajiliwa ni 2,199 sawa na asilimia 130 ukilinganisha na usajili wa mwaka uliopita na usajili  bado ukiendela.

Kuhusu leseni amesema mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya leseni za uvunaji wa mazao ya misitu mbalimbali  3,022 zilitolewa, wakati mwaka wa fedha 2025/2026 kuanzia Julai hadi Machi 13, mwaka huu  zilizokatwa ni 6,898 sawa na asilimia 228.3 na ukataji unaendelea.

“Niwaombe wadau na wananchi kuhakikisha kwamba katika kufanya biashara hizi za mazao ya misitu waweze kuzingatia sheria,kanuni na taratibu ambazo zimewekwa ili  wasiweze kupata changamoto kwenye biashara hizi za mazao ya misitu,”amesema  Mrwana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button