Usugu wa vimelea wapungua, vifo vyashuka

DAR ES SALAAM: Matumizi ya dawa za antibiotiki kiholela yamepungua kwa 80%, hivyo kupelekea pia kupunguza vifo kwa 14% vitokanavyo na usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa binadamu.
Aidha, upande wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa wanyama kumekuwa na juhudi kuhakikisha wafugaji wanahamasishwa kufuga kisasa kwa kuzingatia usafi na kuhakikisha vimelea visiwe chanzo cha maradhi katika mabanda ya mifugo.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Kupambana na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa, Hezron Nonga wakati wa Kongamano la Kuwasilisha Tafiti za Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa lililofanyika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Dar es Salaam.

Nonga ambaye pia ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amesema kumekuwa na kampeni za kuogesha mifugo dhidi ya wadudu wanaong’ata mifugo na kueneza magonjwa hususani kupe na ambao wamekuwa wakipelekea uwepo wa maradhi mengi ambayo yanalazimu matumizi holela ya dawa.
“Kupitia uogeshaji wa mifugo wote nchini ni kwamba tumeona kiwango cha maradhi yale kimepungua kwa kiwango kikubwa na hivyo hata matumizi ya dawa za kutibu mifugo yamepungua lakini zaidi ya yote kumekuwa na kampeni kuchanja mifugo,” amesema Prof Nonga.
Amesema ng’ombe milioni 40 walioko nchini, mbuzi milioni 30, kondoo milioni 10 na kuku milioni 100 walioko tanzania wamepatiwa chanjo.

“Matumizi ya dawa holela katika ngazi ya kaya yamepungua sana kwa hiyo hiyo ni moja ya juhudi kubwa taifa tunajivunia chini ya uratibu wa hii kamati maalumu,” ameongeza Prof Nonga.
Amesema kupitia kampeni hiyo walitoa elimu kwa jamii kwa kuwafahamisha sio kila homa ni ugonjwa unaohitaji dawa za matibabu hivyo ni vyema kwenda hospitali kupima na kupata mwongozo wa madaktari.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utawala wa Fedha na Mipango, Profesa Erasto Mbugi, amesema kuwa taasisi MUHAS chuo hicho kina jukumu kubwa la kufundisha, kufanya utafiti na kutoa huduma za kiafya tiba.

Akizungumza alipomwakilisha akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Appolinary Kamuhabwa, Profesa Mbugi amesema makongamano ya aina hiyo ni muhimu katika kupambana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

“Sasa katika kuhamasisha kupambana huo usugu lazima tufanye warsha za mara kwa mara ili kufanya madaktari wetu tunaowazalisha wajue lakini hata wanaotoa huduma waweze kuwa wanaelewa lakini hata tafiti zetu ziweze kufanyika ili kugundua matibabu mbalimbali ukiwa pamoja na dawa ambazo zinaweza kuwa na nguvu ya kuondoa usugu wa virusi hivyo,” amesema.
Amesema binadamu na vimelea wanatofautiana kwa kuwa miili ya binadamu ni mikubwa hivyo haibadiliki sana, wakati vimelea ni vidogo na vina uwezo mkubwa sana wa kubadilika ili viweze kuishi na mazingira.

Amesema kuwa mojawapo ya njia za vimelea kuishi ni kujikinga na hali inayokutana nayo kwenye miili ya binadamu, ikiwa ni pamoja na mapambano ya madawa na kinga za mwili.
Profesa Mbugi amesema mapambano hayo ndiyo yanavyovifanya vimelea kubadilika badilika na kusababisha usugu.
Amesema warsha hiyo inatoa uelewa kwa watu wa huduma, wanafunzi, jamii nzima pamoja na wanahabari kuhusu matumizi ya dawa kwa utaratibu unaostahili.
Aidha amesema wananchi wanaishi na wanyama wengi wanaowafuga kwa ajili ya kujiongezea kipato, na kwamba usugu unaweza kuenea kutoka kwa wanyama wanaofugwa pamoja na wanyama wa porini.
“Sasa ikitokea kwamba vimelea ambavyo vinaathiri wanyama wa porini, wanyama tunaowafuga, tukala bila kupika vizuri nyama zao au bidhaa zao kama maziwa maana yake kuna uwezekano mkubwa wa vimelea hivyo kuvipata,” amesema.

Akizungumzia chanzo cha maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, amesema historia ya mabadiliko ya kwanza ya magonjwa ilitokana na ufugaji kwa kuwa wanyama wa porini wameishi na wadudu, hivyo wanapoletwa kufugwa huleta pia magonjwa karibu na binadamu.
Amesema kuna mwingiliano mkubwa kati ya wanyama wanaofugwa na binadamu, na katika baadhi ya jamii kama za Kimaasai, kuenea kwa vimelea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu au kutoka kwa binadamu kwenda kwa wanyama ni rahisi zaidi.



