DC Mwenda aendesha zoezi upandaji miti Iramba

Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda leo amewaongoza watumishi na wakazi wa kata ya Old Kiomboi kupanda miti katika Hospital ya Wilaya ya Iramba na Zahanati ya Tutu iliyopo kata ya Kiomboi wilayani humo.

Zoezi hilo ni kuelekea maadhimisho ya kilele cha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambayo huadhimishwa Disemba 9 kila mwaka.

DC Mwenda amesema Wilaya ya Iramba inasherekea maadhimisho hayo kwa kuwakumbusha wananchi kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha wanaienzi amani ili nchi iendelee kubaki salama na kushiriki shughuli za maendeleo popote pale walipo.

“Moja ya jambo kubwa ambalo Kama taifa tunatakiwa kulienzi ni namna ya kuboresha, kuitunza na kuiendeleza amani ya nchi yetu. Ni tunu kubwa ambayo tuko nayo kama taifa ambapo wenzetu maeneo mengi tunu hiyo hawana… Tunaposherekea uhuru wa taifa letu lazima tujue kwamba tunao wajibu kama wananchi wa kushiriki shughuli za maendeleo popote pale,”amesema Mwenda.

Pia Mwenda amesema katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara serikali kwa kushirikiana na wananchi yapo mengi ya kujivunia kimaendeleo katika sekta mbali mbali kichumi kijamii na kitamaduni ikiwa ni matoke ya kupiga hatua katika maendeleo ya nchi.

“Wakati huo wilaya nzima kulikuwa na sehemu tatu tu za kupata huduma za afya…leo hii tunazungumza kila kijiji kuna zahanati, kila kata ina sekondari. Tuna sahemu zaidi ya 54 ambazo zinatoka huduma za afya katika wilaya hii,” ameongezaDC Mwenda.

Aidha DC Mwenda ametoa wito kwa wananchi kuendelea na zoezi la upandaji miti katika msimu huu wa mvua na kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ili iendelee kukua kubaki salama.

Jumla ya miti 900 ya kivuli, miti ya mbao pamoja na miti ya matunda imepandwa. Halmashauri ya Wilaya ya Iramba inaendelea kutekeleza agizo la serikali la kila halmashauri kuhaksikisha inapanda miti 1,500,000.

Habari Zifananazo

Back to top button