MAREKANI : Asilimia kumi ya wafanyakazi wa serikali kuondoka kwa hiari

MAREKANI : RAIS wa Marekani, Donald Trump, ametangaza ofa maalum ya malipo kwa wafanyakazi wa serikali ya Marekani watakaopenda kujiuzuru kwa hiari, katika jitihada za kupunguza idadi ya wafanyakazi na kuongeza tija ya mapato ya serikali.
Katika barua pepe aliyosambaza kwa mamilioni ya wafanyakazi siku ya Jumanne, Trump alisema utawala wake unalazimika kutekeleza mpango huo kuanzia tarehe 6 Februari, ambapo wafanyakazi wanaotaka kushiriki watatakiwa kujisajili.
Ofa hii itawawezesha wafanyakazi wanaoacha kazi kwa hiari kupatiwa mshahara wa miezi minane pamoja na marupurupu mengine kama malipo yao ya kuacha kazi.
Kwa mujibu wa mpango huu, serikali ya Marekani inatarajia kuona asilimia 10 ya wafanyakazi, sawa na takribani 200,000 kati ya wafanyakazi zaidi ya milioni mbili waliopo serikalini, wakikubali ofa hiyo.
Maafisa wakuu wa Trump wamesema kuwa mpango huu unaweza kuisaidia serikali kuokoa dola za Kimarekani bilioni $100.
Zoezi hili linatarajiwa kufanyika hadi tarehe 30 Septemba 2025, ambapo serikali itajua ni kwa kiasi gani wamefanikiwa. SOMA: Trump afungiwa kusitisha ufadhili wa serikali
Wafanyakazi ambao hawatashiriki katika mpango huu ni pamoja na wafanyakazi wa posta, wanajeshi, maafisa wa uhamiaji na usalama wa taifa.



