MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Lindi, Zainab Lipalapi baadhi ya viongozi na wanachama wengine 45 mkoani humo wamejiunga na chama cha ACT Wazalendo.
Viongozi waliojiunga ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA) Mkoa wa Lindi, Said Mzee; Katibu wa Jimbo, Musa Rwegoshora, Mwenyekiti wa Wazee Jimbo, Bakari Likaku, Mweka Hazina wa Jimbo, Mohamed Mandoyo na Mwenyekiti Bavicha Jimbo, Doa Omari.
Soma: Historia ya Mchinjita mpaka kuwa M/Mwenyekiti Bara ACT
Tukio hilo limetokea katika mkutano wa hadhara uliofanyika Lindi Mjini na kuhutubiwa na Makamu Mwenyekiti Taifa wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Rwegoshora amesema ni wajibu wa wanalindi kuwa na jukwaa moja la upinzani na kwamba jukwaa sahihi ni ACT Wazalendo.
Kwa upande wake Mchinjita amewapongeza wanachama wapya na kuwambia kuwa wamechagua jukwaa sahihi kwa kuwa ACT Wazalendo ni chama chenye majawabu ya matatizo na changamoto zinazowakabili watu wa Lindi.