“Amani inaepusha migogoro”

TANZANIA inaendelea kujitolea kikamilifu na iko tayari kufanya kazi na familia ya Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa.” Ni kauli ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York, Marekani.

Dk Mpango alizungumza hayo Septemba 22, 2023 alipomwakilisha Rais Samia katika mkutano huo, ambapo aliongeza kuwa “Umoja wa Mataifa ulianzisha udugu wa kihistoria, undugu, na kujitolea kwa kanuni za kutovurugana, usawa kati ya mataifa, na manufaa ya pamoja, misingi ambayo sasa inapotea.”

Katika mwendelezo wa kuzungumzia amani, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Amani Dunia ambayo imefanyika Septemba 21, Chuo Cha Diplomasia nchini pia kimeadhimisha siku hiyo kwa kusisitiza umuhimu wa amani Tanzania na duniani kote.

Akizungumza katika maadhimisho hayo katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) leo, mgeni rasmi wa tukio hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi amesema kuna umuhimu wa kutunza amani kwani endapo itatoeka hakuna sehemu itayokuwa salama.

Akisisitiza kauli mbiu ya ‘Hatua za Amani, Shabaha Yetu Kwa Malengo ya Dunia’ Balozi Mbundi ameielezea amani kuwa ni sababu ya kuepusha migogoro, lakini pia ili kulinda utamaduni ni lazima pia amani itukuzwe.

“Tunajukumu la kulinda amani, tukikosa amani hakuna sehemu itakuwa salama.” Amesema Balozi Mbundi, huku akitolea mfano wa baadhi ya mataifa ya Afrika ambayo miaka kadhaa nyuma yalikuwa na amani, lakini kwa sasa imetoeka.

Akizungumza katika mahojiano na HabariLEO, mhadhiri msaidizi kutoka Chuo Cha Diplomasia Dar es Salaam, Dennis Konga amesema miongoni mwa juhudi zinazofanyika katika kulinda amani ni pamoja na kutengeneza uchumi wa kujitegemea na kuleta maendeleo binafsi akiamini kuwa chanzo kikubwa cha baadhi ya migogoro duniani ni rasilimali.

Amesema kupitia chuo chao wanafundisha masuala yanayohusu usuluhishi wa migogoro, na diplomasia lengo ni kuijengea jamii bora yenye amani. Amesema vijana wengi Afrika wana mawazo mazuri ya kufanya vitu vikubwa, hivyo kuna umuhimu wa vijana hao kuangaliwa kwa jicho la kipekee katika kutengeneza leo yao iliyo bora.

Konga amesema maadhimisho hayo yamegusia sehemu tatu, nafasi ya taasisi za kimataifa katika kulinda amani duniani, lakini tahadhari ya mapema akimaanisha kuwa kuna baadhi ya viashiria katika baadhi ya nchi kutokuwa na amani, hivyo hakuna haja ya mataifa ya nje kukomesha viashiria hivyo kwani Afrika inaweza kuwajibika katika hilo.

“Mwisho ni kuangalia nafasi ya nchi katika huo mchakato wa kuleta amani, na hii ipo tangu miaka ya nyuma, wakati wa Mwalimu Nyerere alipozungumza tutawasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili kuangaza kwenye giza, tuleta amani kwenye unyonge, tulete faraja na huu ndo mchango wa Tanzania katika maeneo mengi.” Amesema Konga.

3 comments

Comments are closed.