UONGOZI wa klabu ya Azam umesema upo katika mipango ya kikosi cha timu hiyo kwenda kuweka kambi nje nchi kipindi ambacho Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi na Ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wa ndani(CHAN) kwa timu ya taifa.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Azam, Hashim Ibwe timu hiyo imepata mialiko Afrika Kusini, Zambia, Qatar na Dubai na kwamba kati ya nchi hizo wanaangalia nchi gani kwao ina manufaa kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
“Wachezaji wamepewa mapumziko mafupi na viongozi wanaangalia katika mialiko tuliyopata ni nchi ipi wataridhia na ina tija kwetu na kwenda kuweka kambi kwa kipindi chote,” amesema.
Ibwe amesema kipindi cha mapumziko ya ligi hiyo kocha Rachid Taoussi amepanga timu icheze mechi tatu hadi nne za kirafiki kwa ajili ya kujiimarisha zaidi.
“Mechi hizo zitawapa nafasi ya wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza duru la kwanza lakini pia waliotoka kwenye majeraha nao waweze kupata mechi za ushindani kujenga utimamu wa mwili,” amesema Ibwe.