Baadhi ya maeneo kukosa mvua za vuli
MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imesema katika msimu wa mvua za vuli mwaka 2024 maeneo mengi yanatarajiwa kukosa mvua.
Hali ya joto la bahari katika eneo la kati la kitropiki, la bahari ya pasifiki, inatarajiwa kuwa chini ya wastani hali ambayo inaashiria uwepo wa Lanina.
Akitoa taarifa hiyo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dk Ladislaus Chang’a amesema katika maeneo mengi mvua zitakuwa za kusuasua.
SOMA: Hali tete ongezeko hali mbaya ya hewa
Amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba na wiki ya pili ya Oktoba na zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba.
Kutokana na uchache huo wa mvua wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayostahimili ukame, pamoja na matumizi mazuri ya akiba ya chakula kilichopo hapa nchini.
View this post on Instagram
Dk Chang’a amesema ipo haja ya mamlaka mbalimbali nchini kuchukua hatua kunusuru sekta wanazozisimamia ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea ikiwemo magonjwa kwa binadamu, wanyama, pamoja na upungufu wa chakula.
SOMA: Watakiwa kuchukua hatua uwepo wa El Nino
Kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi za mikoa wilaya kata na vijiji zimeshauriwa kutoa elimu ya kukabiliana na athari zitakazo sababishwa na upungugu wa mvua za vuli.
Amesema katika kuhakikisha taarifa hizo zinafanyiwa kazi, waandishi wa habari wametakiwa kutumia kalamu zao ipasavyo, kwa kuandaa taarifa za kisekta kuhusu matumizi ya utabiri wa hali ya hewa ikiwemo madini nishati, uvuvi na afya.