Bajeti yakonga mioyo ya wananchi

SERIKALI imepongezwa kwa kuwasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi, hatua inayoonekana kuwa chachu kwa sekta ya fedha hususani mabenki kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO baada ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kuwasilisha bajeti ya Sh trilioni 56.4 juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Akiba, Silvest Arumasi alisema bajeti hiyo inaakisi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na bajeti ya mageuzi jumuishi inayowajumuisha wananchi wote.
Arumasi alibainisha kuwa bajeti hiyo imelenga maeneo makuu mawili; kuendeleza uwekezaji katika miradi ya kimkakati inayochochea uchumi, na kuimarisha uwezo wa serikali kukusanya mapato ya ndani.
Alisema bajeti ya mwaka huu imeongezeka kwa takribani Sh trilioni sita ambazo zaidi ya Sh trilioni nne zinatokana na makusanyo ya ndani, jambo linaloonesha dhamira ya serikali kujitegemea kifedha.
Aidha, alipongeza hatua ya serikali kupunguza kodi kwenye miamala ya kielektroniki kutoka asilimia 18 hadi 16, akisema hatua hiyo itahamasisha wananchi kutumia njia za malipo ya kidijiti badala ya fedha taslimu.
Alisema, “Unapohamasisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki, benki zinafanya kazi kwa ufanisi zaidi, wafanyabiashara wanapunguza hatari ya wizi wa fedha taslimu na wananchi wanakuwa na uhakika wa kufikia huduma za kifedha”.
Aliipongeza serikali kwa kuzuia mamlaka mbalimbali kufunga biashara kwa sababu ya changamoto za kisheria, na badala yake kutafuta njia ya kusuluhisha migogoro.
Alisema hatua hiyo inalinda wajasiriamali waliokopa benki na inaimarisha mazingira ya biashara.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema bajeti hiyo imeipa nguvu sekta ya usafirishaji na imeweka mazingira ya kukamilika kwa vipande vyote vitano vya Reli ya Kisasa (SGR) vinavyoendelea kujengwa.
Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Shukuru Manya alisema ameridhishwa na msisitizo uliowekwa katika kuendeleza miradi ya kimkakati kama SGR pamoja na kuendelea kwa ruzuku ya mbolea kwa wakulima, hatua itakayoongeza tija kwenye kilimo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko (Chadema) alisema bajeti imeonekana kugusa maisha ya wananchi wa kawaida hasa baada ya kuondolewa kwa kodi nyingi kwenye bidhaa za kilimo, jambo alilosema linaonesha
dhamira ya serikali kuwafikia watu wa kipato cha chini.
Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo alieleza kuwa bajeti hiyo imezingatia maslahi ya waendesha bodaboda kwa kupunguza baadhi ya kodi na ushuru, sambamba na kuondoa baadhi ya tozo kwa watalii, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya serikali.
Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli alisema ongezeko la kodi kwenye vinywaji ni hatua ya makusudi inayolenga kuimarisha sekta ya afya kwa kutoa fedha za bima ya afya kwa wote na upatikanaji wa dawa kwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi.
Pia, alipongeza msukumo wa serikali katika makusanyo ya fedha kupitia mafuta na maeneo mengine muhimu. Katika Mkoa wa Mara, wananchi walipokea bajeti hiyo kwa mitazamo tofauti wakisisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo ni jambo muhimu zaidi.
Wamesema bila usimamizi mzuri, uwazi wa matumizi, na ushirikishwaji wa wananchi, mafanikio ya bajeti hiyo yatakuwa finyu.
Mwanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Daniel Raphael alisema bajeti imeonesha mwelekeo chanya katika elimu ya juu, lakini akasisitiza kuwa vijana wanahitaji kuona matokeo halisi kama ajira.
Dereva bodaboda katika Kata ya Nyasho, Charles Gorge alisema kodi na tozo bado ni mzigo kwa watu wa kipato cha chini. Mkazi wa Kata ya Bweri, Fatuma Shilinde alipongeza bajeti kwa kugusa afya ya uzazi na uwezeshaji wa wajasiriamali.
Alisisitiza umuhimu wa elimu ya kutosha juu ya namna ya kufikia mikopo ili wananchi wafaidike moja kwa moja.
Kwa ujumla, bajeti ya 2025/2026 imepokelewa kwa pongezi lakini pia kwa tahadhari, huku angalizo likitolewa katika kusimamia utekelezaji wake, usimamizi wa matumizi ya fedha na kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.