Bandari ya Dar kuimarisha usafirishaji wa mazao

DODOMA — Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema kuwa Serikali imetenga eneo maalum kwa ajili ya kuboresha huduma za usafirishaji wa mazao ya mbogamboga, mifugo na matunda kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Abdallah Shangazi, kuhusu lini bandari hiyo iliyoboreshwa itaanza kusafirisha shehena hiyo, Naibu Waziri Kihenzile amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilitenga Kiwanja Na. P28 chenye ukubwa wa mita za mraba 239,053 kilichopo Kurasini, Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa eneo hilo linakusudiwa kutumika kwa shughuli za kibandari ikiwa ni pamoja na kuhifadhi makasha, kupanga na kukusanya shehena, kuhudumia bidhaa zinazoharibika haraka kama mbogamboga na matunda, pamoja na kuwa sehemu ya maegesho ya malori yanayosubiri kuingia bandarini.

“Mpango wa matumizi ya eneo hilo pamoja na usanifu wa kina vimekamilika, na sasa TPA ipo katika hatua za kutafuta rasilimali fedha ili kuanza ujenzi,” alisema Naibu Waziri Kihenzile.

Ameongeza kuwa kwa sasa, usafirishaji wa mazao hayo unafanyika kupitia makasha maalum ya kuhifadhia bidhaa zinazoharibika haraka (reefer containers) yaliyopo katika Bandari ya Dar es Salaam. Serikali imepanga kuongeza idadi ya makasha hayo maalum ili kukidhi mahitaji ya soko ambayo yanaendelea kuongezeka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button