Benki yaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa
BENKI ya I&M imeadhimisha kumbukizi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1974.
Maadhimisho hayo yamefanyika wiki hii makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Group PLC, Sarit Raja-Shah ameeleza namna wanavyojivunia utendaji wa benki hiyo na kuisaidia jamii katika masuala mbalimbali ya kifedha.
Pia amesema maadhimisho yao wameangazia chimbuko la benki hiyo, ilipotoka, inakoelekea na ukuaji wake wa kasi.
“Maadhimisho haya ni uthibitisho wa ukuaji wa benki katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na hii ni ishara ya mchango wa Benki ya I&M Tanzania katika uchumi na watu wa Tanzania, ofisi yetu hii mpya haiwakilishi tu ukuaji wa benki yetu, lakini pia ni dhamira yetu inayoendelea ya kutoa huduma zenye ubora na ufanisi, ” alisema Raja-Shah.
SOMA: Benki yazindua huduma maalum kwa wastaafu
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania, Zahid Mustapha ameeleza kuwa katika miongo mitano iliyopita, benki hiyo imeonesha nia ya dhati ya kutoa huduma zenye ubora zinazotumia teknolojia ya kisasa na zinazochagiza maendeleo ya jamii.
Amesema maadhimisho kama hayo pia yamefanyika kwenye nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kwa heshima ya safari ya mafanikio ya benki hiyo tangu kuanzishwa kwake hadi kuwa moja ya watoa huduma wakuu wa huduma za kifedha Afrika Mashariki.
SOMA: Benki yazindua akaunti ya mfugaji
“Tunawapongeza wateja wetu wote na tunawatambua kutokana na mchango na uwekezaji wao katika benki hii ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi na hii inatupa deni sisi watendaji tuendelee kujituma ikiwemo kuboresha huduma zetu ili waweze kupata kilicho bora zaidi,” alisema Mustapha.