Bil 23/- zaendeleza elimu msingi, sekondari Meatu

SIMIYU: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema jumla ya Sh bilioni 23.98 zimetolewa kwa ajili ya kuiendeleza sekta ya elimu wilayani Meatu mkoani Simiyu katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.
Akizungumza na wananchi wa Meatu mkoani humo katika Kiwanja cha Stendi ya Mabasi Meatu kwenye muendelezo wa ziara yake ya siku tano Simiyu, Rais Samia amebainisha kuwa uwekezaji huo unajumuisha Sh bilioni 8.64 zilizotolewa kwa ajili ya kufanikisha elimu bila malipo, suala ambalo limeongeza idadi ya wanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari.
“Uwekezaji huo umeongeza idadi ya wanafunzi wa sekondari kutoka 9, 458 mwaka 2022 hadi 12, 630 mwaka 2025, huku wanafunzi 9,599 wakiandikishwa kwa ajili ya elimu ya awali, Wanafunzi 11, 000 wakiandkishwa darasa la kwanza bila mchango wowote kutoka kwa wananchi. Hii ni kazi ya serikali ya awamu ya sita,” amesema Rais Samia.
SOMA ZAIDI
Aidha, akizungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Rais Samia amebainisha kuwa takribani milioni 799 zimetolewa na Halmashauri ya Meatu kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu tangu mwaka 2021, akiipongeza halmashauri hiyo kwa uwezeshaji huo na kuitaka kuongeza kasi zaidi katika kutoa huduma za mikopo kwa Jamii.
Rais Samia pia kwa kutambua shughuli ya kiuchumi ya ufugaji kwa wananchi wa Meatu ameeleza kuwa serikali yake tayari imeanzisha kituo cha wakala wa maabara ya wanyama wilayani humo ili kupima na kubaini magonjwa ya mifugo, akitoa wito pia wa ushiriki wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo, aliyoizindua Jana Jumatatu Juni 16, 2025 Bariadi Mjini.