WACHIMBAJI wadogo wa madini nchini hasa vijana na wanawake wataanza kunufaika na programu ya kuboresha mazingira ya uchimbaji madini, inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa thamani ya shilingi bilioni 30.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imefanikisha Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi nne za Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) zitakazonufaika na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Madini inayotekelezwa kwa ubia kati ya OACPS na EU.
Programu hiyo inatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2022 hadi 2024 kwa ufadhili wa Euro milioni 11.1 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 30, kutoka Umoja wa Ulaya.
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/25 imeainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo chama kitaendelea kuisimamia serikali kuhakikisha mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya madini yanaendelezwa.
Ilani hiyo inaeleza kuwa chama kitahakikisha wananchi wanawezeshwa kuwa sehemu ya umiliki wa rasilimali madini na hiyo na hivyo kuchangia pato la taifa na kupunguza umasikini nchini.
Ilani hiyo imefafanua kuwa ili kufikia malengo hayo itasimamia serikali kubuni na kuimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija.
Aidha, imebainisha kuwaendeleza kutoka uchimbaji mdogo kwenda wa kati na hatimaye uchimbaji mkubwa na kuwapa mafunzo yanayohitajika kuhusu uchimbaji na biashara ya madini.
Akiwasilisha bajeti ya wizara bungeni, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alisema kupitia programu hiyo, sekta ya madini nchini itanufaika na miradi ya kuendeleza wachimbaji wadogo hususani vijana na wanawake.
Balozi Mulamula alisema hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo; na kuwa nchi nyingine tatu zilizonufaika kuingia kwenye programu hiyo ni Suriname, Burkina Faso na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika hotuba yake hiyo Balozi Mulamula alisema wizara hiyo imechukua hatua mbalimbali katika kusimamia na kuratibu masuala ya uhusiano baina ya Tanzania na nchi nyingine ikiwemo jumuiya za kimataifa.
“Katika eneo la Ushirikiano wa Tanzania na Nchi za Ulaya na Amerika, yapo mengi tuliyofanya na yanayoendelea kufanywa na ninafurahi kusema, tumefanikisha Tanzania kuchaguliwa kuwa mnufaika wa programu ya (OACPS) katika sekta ya madini.”
Akizungumzia programu hiyo alisema itawajengea uwezo wachimbaji wadogo hususani vijana na wanawake katika sekta hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu hadi 2024.
Utekelezaji wa programu hiyo utachochea sekta ya madini katika nchi za OACPS kutoa mchango stahiki katika kuongeza mnyororo wa thamani ya madini, uzalishaji wa nafasi za ajira na ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla.
Balozi Mulamula alisema upatikanaji wa nchi za kunufaika na awamu ya pili ya programu hii ulioanza mchakato wake mwezi Agosti mwaka jana, ulikuwa na ushindani mkubwa kutokana na idadi kubwa ya nchi zilizoomba kujumuishwa kwenye programu hiyo.
Jumuiya ya OACPS ina jumla ya nchi 79, hivyo kuchaguliwa kwa Tanzania kunufaika na programu hiyo ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa ushawishi wa Tanzania ndani ya Jumuiya ya OACPS na kazi nzuri inayofanywa na serikali katika kuimarisha ushirikiano na jumuiya hiyo kupitia wizara hiyo na Ubalozi wa Tanzania ulioko Brussels, Ubelgiji.
Utekelezwaji wa programu hii utafanywa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Wizara ya Madini chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
Serikali kupitia Wizara ya Madini inajiandaa ipasavyo kuanza utekelezaji wa programu na tunatoa rai kwa wadau wa sekta ya madini hasa wachimbaji wadogo kuchangamkia ipasavyo fursa zitakazotokana na programu hiyo.
Juni mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Joseph Sokoine alihudhuria mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa OACPS mjini Brussels na kusema Tanzania itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya OACPS kuhakikisha vipaumbele vya nchi vinatekelezwa.
Alitaja vipaumbele hivyo ni sekta ya madini, kilimo, viwanda na biashara na uvuvi.
Akizungumzia vipaumbele vya Wizara ya Madini, Dotto Biteko kwa mwaka 2022/23, wakati akiwasilisha bungeni bajeti ya wizara hiyo alisema mkakati upo wa kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa madini.
Alisema katika kipengele hicho, wizara itaimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo au kuwapatia leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa za msingi za kijiolojia.
Biteko alisema wizara kwa mwaka 2022/23 itawaendeleza wachimbaji wadogo kuwa wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa kwa kuwapa mafunzo yanayohitajika kwenye uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini.