“Bima ya Afya kwa wote itekelezwe haraka”

SERIKALI imeweka mkakati  kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inaanza kutekelezwa haraka kwa kuwa imeshawekeza kwenye miundombinu, vifaa, vifaa tiba, dawa pamoja na ujuzi wa madaktari wanaotoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amezungumza hayo Oktoba 30, katika Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kitaifa la Ugharamiaji wa Huduma za Afya linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha.

“Lazima tufike mahali tukubali kuwa na Bima ya Afya kwa Wote kwa maana tumewekeza kwenye miundombinu, vifaa, vifaa tiba, dawa pamoja na ujuzi kwa madaktari wetu ili wananchi wanapotaka kupata tiba wapate kwa haraka na wepesi,” amesema Waziri Mhagama.

Advertisement

Ameongeza kuwa ili kufanikisha jambo hilo lazima Serikali ishirikiane na Sekta Binafsi lakini pia kuendelea kuboresha ubora wa huduma kuanzia kwenye afya msingi hadi taifa, kuimarisha mifumo ya rufaa ambayo inaweza kupatikana kwa Watanzania wote pamoja na kuzingatia weledi na uzalendo wa watoa huduma.

Waziri Mhagama amesema kwa sasa madaktari bingwa wa Rais Samia wameanza kuzunguka nchi nzima kuhakikisha kuwa huduma za afya zinawafuata wananchi kila mahali kwa gharama nafuu. “Kwa sasa wamefikia Halmashauri karibu zote nchini, huku wananchi zaidi 122,320 wakiwa mamepatiwa huduma na wengine zaidi ya 8,018 wakiwa wamefanyiwa upasuaji mbalimbali kwa mafanikio mazuri,” amesema.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Jackline Kahinja (Mb) amesisitiza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote ambapo kamati hiyo itasimamia vilivyo sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

“Tutahakikisha tunafuatilia kwa kina vyanzo vyetu vya mapato ya ndani ili kuwawezesha watu wasio na uwezo waweze pia kupata huduma za afya bila malipo,” amesema Kahinja.

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dk Charles Mosses amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni ushahidi tosha kuwa Tanzania inatekeleza kwa vitendo utoaji huduma bora za afya kwa wananchi wake. “Jambo zuri ni kwamba kwamba bima hii pia imeweka kipengele maalum cha huduma kwa watu wa chini hususani wale ambao hawana uwezo kabisa wa kifedha,” amesema Dk Mosses.

SOMA: Wataaamu wa afya kujengewa uwezo