Biteko ataka uhuru Afrika uzalishaji nishati

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametoa wito kwa nchi za Afrika kupewa uhuru wa kuzalisha nishati kwa kutumia rasilimali zilizopo barani humo.
Dk Biteko ametoa wito huo jana wakati akizungumza katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St Petersburg linalofanyika nchini Urusi.
Alisema Afrika inahitaji programu itakayosaidia kufikia dhamira yake ya kuondoa idadi kubwa ya watu ambao hawatumii nishati safi. Alitaja baadhi ya athari za matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo uharibifu wa mazingira.
Akitolea mfano Tanzania, Dk Biteko alisema Afrika ina vyanzo vingi vya kuzalisha nishati. Alitaja vyanzo vya nchini ni jua, maji na gesi asilia.
Hata hivyo alisema barani humo hakuna uhuru wa kutumia makaa ya mawe licha ya kuwepo kwa kiwango kikubwa pamoja na kuwa nchi kubwa duniani zinaweza kufanya hivyo.
“Hivyo iangaliwe namna kwa kila nchi kutumia rasilimali zake ili kuzalisha nishati, mfumo uliopo unazifanya nchi zote kuwa sawa lakini ukweli ni kwamba hatuko sawa. Kwa mfano Afrika inachangia asilimia tatu hadi nne pekee ya uchafuzi wa mazingira, lakini imepewa mzigo mkubwa zaidi,” alisema.
Alisisitiza, “Kila nchi itumie utaratibu wake wa kuzalisha nishati lakini kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa mazingira.”
Alizungumzia uhusiano mzuri uliopo wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi na kusema kuwa uendelee kuwa wa kuheshimiana na kukubaliana.
Alitaja manufaa yake kuwa ni pamoja na kubadilishana ujuzi na kuisaidia Tanzania katika mitaji ya miradi ya nishati.
Alibainisha kwamba Tanzania ina mpango wa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha takribani megawati 120 za umeme.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Urusi, Sergey Tsivilev alisema kuwa Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin amekuwa na jitihada za kuhakikisha inaungana na nchi nyingine katika kupatia ufumbuzi changamoto za nishati.