Bodi ya Ithibati yaongeza muda kujisajili hadi Juni 28

BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeongeza muda wa kujisajili kwenye mfumo wa TAI-Habari wa siku saba mpaka Juni 28.

Awali, kulingana na tangazo la awali la JAB, jana ndio ulikuwa muda wa ukomo wa waandishi kujisajili kwenye mfumo kwa ajili ya kupata vitambulisho maalumu vitakavyowawezesha kukusanya na kuchakata habari.

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa bodi hiyo, Patrick Kipangula kwa vyombo vya habari jana ilisema lengo la kuongeza muda ni kutoa nafasi kwa waandishi ambao wamekamilisha usajili lakini hawajalipa ada ya ithibati na kuwapa fursa wale ambao walianza usajili na hawajakamilisha.

“Bodi inawahimiza waandishi wa habari wote nchini kutumia muda huu ipasavyo kujisajili, baada ya muda huo kuisha, waandishi watakaoshindwa kujisajili hawataruhusiwa kufanya kazi za kihabari kwa kufanya hivyo ni kinyume cha masharti ya kifungu cha 19 cha sheria ya huduma za habari sura ya 229,” alisema.

Alisema bodi inatoa onyo kali kwa mtu yeyote atakayewasilisha vyeti vya kughushi au taarifa za uongo katika mchakato wa usajili.

“Kitendo hicho ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema.

Alisema bodi itaendelea kuhakiki vyeti na kutoa vitambulisho kwa waandishi wa habari waliotimiza vigezo kwa mujibu wa sheria na hata baada ya muda wa usajili kumalizika.

“Usajili huu ni hatua muhimu katika mchakato wa kuanzishwa kwa baraza huru la habari kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 24 cha sheria ya huduma za habari sura ya 229,” alisema.

Aidha, alisema kwa kuzingatia uwepo wa uchaguzi mkuu mwaka huu na kwa mujibu wa masharti ya kanuni ya 12 (g) ya kanuni za utangazaji wa uchaguzi kwa vyama vya siasa, waandishi wa habari ambao ni wagombea wa nafasi za kisiasa wazingatie kutojihusisha na majukumu yoyote ya kihabari katika vyombo vya habari walivyoajiriwa kwa muda wote wa mchakato wa uchaguzi.

“Hatua hii inalenga kuzuia mgongano wa maslahi na kulinda uaminifu wa vyombo vya habari mbele ya umma hususan katika kipindi cha uchaguzi,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button