Bunge la 12 kuhitimishwa leo

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuhitimisha Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli alizindua bunge hilo Novemba 13, 2020 jijini Dodoma kwa kuzingatia Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi alisema bungeni kuwa leo Rais Samia atahutubia bunge na kuhitimisha shughuli za Bunge la 12.
Katika kikao cha 54 cha Bunge la 19 Juni 26, lilitengua kanuni ya 160 (1) na kanuni ya 164 (f) ili kuruhusu wageni walioalikwa na Spika wa Bunge waingie bungeni kusikiliza hotuba ya Rais Samia.
Wengi wa wabunge katika bunge hilo walichaguliwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020 na Spika wake wa kwanza alikuwa Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai na sasa linavunjwa likiongozwa na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema bunge hilo limefanya kazi kwa bidii.
“Tumetafakari hoja, tumejadili miswada na tumetoa maazimio yenye tija kwa maendeleo ya nchi yetu. Ni wakati sasa wa kurejea majimboni ili kujiandaa na uchaguzi mkuu, ni matumaini yangu wananchi watatupa ridhaa kwa mara nyingine,” alisema Majaliwa bungeni Dodoma wakati akitoa hoja kuahirisha Mkutano wa 19 wa bunge hilo.
Alisema wakati wa Bunge la 12, maswali ya msingi 5,259 na maswali ya nyongeza 18,075 na maswali 253 ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na wabunge na kupatiwa majibu na serikali.
Majaliwa alisema bunge hilo lilijadili na kupitisha miswada 58 kwa hatua zake zote, lilijadili na kupitisha maazimio 19 ya bunge yakiwemo manne ya pongezi, liliridhia mikataba na itifaki 12 na masuala ya maliasili matatu.
“Bunge lako tukufu lilipitisha maazimio 922 yanayotokana na taarifa za kamati za mwaka yaliyohitaji kutekelezwa na serikali wakati wa uhai wa bunge. Vilevile serikali imetoa taarifa 15 kupitia kauli za mawaziri bungeni kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa mambo tofauti yenye maslahi mapana kwa taifa,” alisema.
Matukio yaliyotikisa
Miongoni mwa matukio yaliyotikisa katika uhai wa Bunge la 12 ni pamoja na kujiuzulu kwa aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Dk Tulia Ackson akiwa ni mwanamke wa pili kupewa jukumu hilo, akitanguliwa na Anne Makinda.
Pia, wakati wa Bunge la 12 aliteuliwa Katibu wa Bunge wa kwanza mwanamke, Nenelwa Mwihambi. Wakati wa uhai wa bunge hilo, kulikuwa na vifo vya wabunge 10.
Nao ni Atashasta Nditiye (Muhambwe), Elias Kwandikwa (Ushetu), Franscis Mtega (Mbarali), William Ole Nasha (Ngorongoro) na Khatib Said Haji (Konde).
Wengine ni Mussa Hassan Mussa (Amani), Ahmed Yahya Abdulwakil (Kwahani), Dk Faustine Ndugulile Kigamboni), Irene Ndyamkama na Martha Umbulla wa viti maalumu.
Katika Bunge la 12, uliwasilishwa Muswada wa Maboresho ya Uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mara ya kwanza katika bunge hilo, wabunge 19 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliapishwa katika viwanja vya bunge.
Tukio lingine ni la wabunge watatu waliopewa adhabu ya kutohudhuria vikao na mikutano ya bunge baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali.
Walioadhibiwa ni Luhaga Mpina (Kisesa), Jerry Silaa (Ukonga) na Josephat Gwajima (Kawe). Rais Samia alimteua Mbunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Vilevile, lilitokea janga la Covid-19 lililolazimu wabunge kufanya mikutano kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni tofauti na ilivyo kawaida kulingana na kanuni za bunge.
Aidha, Bunge la 12 ilianzisha utaratibu wa kufanya kazi zake kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa jambo lolote lililohusu bunge, ukiwemo upatikanaji wa taarifa wakati wa vikao vya bunge.
Aprili 4, 2022, Dk Tulia alitangaza kurudishwa kwa matangazo ya moja kwa moja akisema ni dai na hitaji la wananchi.
Wakati wa Bunge la 12, hakukuwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, badala yake kwa kutumia kanuni za bunge zilizorekebishwa ilitambuliwa kambi ya walio wachache.
Samia ahutubia bunge
Aprili 22, 2021, Rais Samia alihutubia bunge hilo kwa mara ya kwanza mwezi mmoja baada ya kuapishwa Machi 19,2021 kuwa Rais wa Awamu ya Sita baada ya kifo cha Rais Magufuli mwezi Machi 17, 2021.
Rais Samia aliwaeleza wabunge kuwa uongozi wake ungedumisha yaliyopita, kuendeleza mazuri yaliyopo na kujenga mapya. Aliahidi kudumisha amani, umoja na mshikamano, uhuru wa nchi na Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano.
Rais Samia alisema angefanya juhudi kusimamia ukuzaji uchumi. Alisema kwa mujibu wa wataalamu, ili kupambana na umasikini uchumi unatakiwa ukue angalau kwa asilimia nane kwa mwaka.
Alisema ni muhimu kuboresha sera za uchumi wa jumla na sera za fedha kuhakikisha viashiria vyote vya uchumi ikiwemo thamani ya sarafu, mfumuko wa bei na viwango vya riba vinabaki kwenye utulivu na asingevumilia wizi, uzembe na ubadhirifu wa fedha za umma.
Rais Samia alisema pia ni muhimu kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia sekta binafsi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Aliahidi serikali yake kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Kigoma.
Aliahidi kujenga barabara katika maeneo ya kimkakati, kukamilisha ujenzi wa madaraja makubwa likiwemo la Kigongo Busisi (JP Magufuli), Daraja la Wami, Daraja la Pangani na Daraja la Tanzanite.