CCM Arusha yapitisha madiwani 160 kugombea

ARUSHA : CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha kimepitisha madiwani 160 kupeperusha bendera ya chama hicho katika majimbo saba ya mkoa huo kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Ramsey Saipurani alisema wagombea waliopitishwa walichaguliwa kwa kuzingatia vigezo vya uadilifu, uchapakazi, uzoefu, historia ndani ya chama na kukubalika kwa wananchi.

Saipurani aliwataka wanachama wa CCM kuwa wamoja wakati wa kampeni na kuwaunga mkono wagombea walioteuliwa, akisisitiza kuwa muda wa malumbano umepita na sasa ni wakati wa kuimarisha mshikamano ili chama kipate ushindi kwa kishindo.

Katika Jimbo la Arusha Mjini, Kata ya Olasiti haijapata mgombea rasmi wa udiwani kutokana na sintofahamu miongoni mwa wagombea, ambapo suala hilo limepelekwa kwa ngazi za juu za chama kwa maamuzi zaidi.

Aidha, alisema katika nafasi ya madiwani wa viti maalumu katika Tarafa ya Elerai, kumekuwa na malalamiko ambayo pia yamewasilishwa kwa vikao vya juu vya chama kwa ajili ya uamuzi wa mwisho. SOMA: “Arusha Mjini wajitokeze uchaguzi mitaa”

Taarifa hiyo inaonesha katika Jimbo la Arusha Mjini, madiwani 14 wa zamani hawakupitishwa, na nafasi hizo zimepewa wagombea wapya. Kata hizo ni pamoja na Moshono, Olmot, Sombetini, Sekei, Ngarenaro, Themi, Engutoto, Terat, Muriet, Sokoni One, Sinoni, Sakina, Levolosi na Lemara.

Kwa upande wa Jimbo la Longido, Katibu Mwenezi wa wilaya hiyo, Solomoni Lekui alieleza madiwani sita wa zamani pia hawakupitishwa kutokana na kushindwa kushika nafasi za juu kwenye kura za maoni au kukosa sifa za kimaadili. Kata hizo ni Kamwanga, Engikaret, Namanga, Engarenaiobo, Ketumbeine na Iloirienito.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button