CCM Kigoma yaridhishwa utekelezaji Ilani

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kigoma imepitisha kwa kauli moja Azimio la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020.
Mwenyekiti wa CCM Kigoma, Jamal Tamim ametangaza azimio hilo la wajumbe wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika Mjini Kigoma ambapo amesema wajumbe wameridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na serikali kutekeleza miradi ambayo inagusa maisha ya wananchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kigoma Jamal Tamim (katikati aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao cha halmashauri ya CCM Mkoa Kigoma kilichokuwa kikipokea taarifa ya ilani ya uchaguzi ya CCM katika utekelezaji wa miradi
Soma zaidi: CCM Iringa yakana kauli tata ya mwenyekiti halmashauri …
Tamim amesema kuwa wakati wakimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa aliyofanya katika utekelezaji wa miradi pia wamempongeza Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye na watendaji wa serikali mkoani humo zikiwemo halmashauri za mkoa huo kwa utekelezaji na usimamizi thabiti wa miradi ambao umeleta matokeo chanya katika maisha ya wananchi wa kawaida.

Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye akizungumza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi kwa wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Mkoa Kigoma ikiwa ni kueleza taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Abdulkadri Mushi pamoja na kuunga mkono azimio hilo na kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika utekeleza wa miradi viongozi wa CCM wa ngazi zote mkoani humo kupitia kamati za siasa za mkoa na wilaya hawana budi kubeba ajenda ya kwenda kwa wananchi kueleza mambo mazuri yaliyofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi ambayo inalengwa kuwakwanua wananchi na kuwaweka hali nzuri ya kiuchumi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Abdulkadri Mushi akizungumza katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa Kigoma iliyokaa kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.
Soma zaidi: Viongozi CCM Iringa wanolewa udereva
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa miradi iliyofanywa mkoani humo Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana Mkoa Kigoma umepokea kiasi cha Sh bilioni 87.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na kwamba miradi hiyo imeleta matokeo chanya kwenye maisha ya wananchi kiuchumi.



