CCM yataka umeme megawati 8,000

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinataka uzalishaji umeme nchini ufikie megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030 inaeleza chama hicho kinatambua umeme ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii na una mchango na nafasi ya pekee ya kupunguza umasikini.
CCM imeleeza katika kipindi cha mwaka 2025 – 2030 itaendelea kuisimamia serikali iongeze kasi ya uzalishaji wa umeme na kuimarisha usambazaji wake.
Ilani hiyo inaeleza chama hicho kinataka kuongeza matumizi ya uhakika ya umeme kwa mtu kutoka kilowati 103 hadi kufikia kilowati 300 ifikapo mwaka 2030 kwa kuimarisha uzalishaji wa umeme kutoka megawati 3,077.96 mwaka jana hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
CCM imeeleza itaisimamia serikali iimarishe mifumo ya usafirishaji wa umeme kutoka kilometa 7,745.4 mwaka jana hadi kilometa 13,366.85 mwaka 2030.
Chama hicho kinataka mifumo hiyo iimarishwe kupunguza upotevu wa umeme wakati wa usafirishaji kutoka asilimia 16 mwaka jana hadi asilimia 10 mwaka 2030 na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya kimkakati ikiwamo mashambani na viwandani.
CCM pia itaisimamia serikali ikamilishe usambazaji wa umeme nchini ikiwa ni pamoja na kupeleka umeme katika vitongoji 31,532 vilivyosalia sawa na asilimia 49 ya vitongoji vya Tanzania Bara na kuunganisha umeme katika kaya na taasisi.
Pia, serikali itasimamiwa iimarishe uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa kwa kushirikisha sekta binafsi.
CCM inataka kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya uendeshaji wa treni ya kisasa ya umeme (SGR) kwa kujenga njia za kusafirisha umeme msongo kilovoti 220 kutoka Makutopora hadi Tabora; Tabora hadi Isaka, Mwanza hadi Isaka na Tabora hadi Kigoma.
Ilani imeeleza kuwa chama hicho kitaisimamia serikali ihamasishe tafiti, bunifu na uwekezaji katika teknolojia zinazohusu uzalishaji wa nishati mbadala ukiwamo wa jua, upepo na mawimbi ya bahari.
Serikali itaagizwa iweke mfumo mpya wa kisera, kisheria na kikanuni utakaotoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa huduma ya umeme.
Pia, CCM itaagiza kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha asilimia isiyopungua 50 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2030.
Serikali itaagizwa ihamasishe matumizi na uwekezaji wa nishati safi ya kupikia kwa kuweka vivutio ili kuimarisha matumizi ya nishati hiyo.
CCM itaisimamia serikali ipunguze gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia na kutoa elimu ili kuwezesha wananchi hususani wa kipato cha chini kutumia nishati safi.