Chalamila atoa maelekezo matumizi nishati safi
DAR ES SALAAM; MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameagiza taasisi zote za serikali kuchangia mitungi ya gesi kuanzia 200 hadi 300 na kuiwasilisha katika ofisi ya mkoa ili kuunga mkono matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kila jitihada za kuhakikisha wanawake wanakuwa salama na kuepuka matumizi ya nishati chafu kwa kuwa ina madhara makubwa kwa binadamu.
Chalamila amesema hayo Dar es Salaam leo katika uzinduzi wa kongamano la matumizi ya nishati safi ya kupikia lililofanyika katika Viwanja vya Karimjee.
“Kila taasisi ya serikali kabla ya kufika Septemba 30 mwaka huu ichangie mitungi ya gesi kuanzia 200 hadi 300, nimeona watu wa mazingira mpo na wengine wote hakikisheni mnalifanyia kazi hili kuwanusuru wanawake na nishati chafu kwani mitungi hiyo itagawiwa kwa kila mwanamke,”amesema.
Soma pia: “Ifikapo 2034 asilimia 80 watumie nishati safi”
Amemuagiza Katibu tawala mkoa kuviandikia barua vyuo vikuu mkoa wa Dar kuchangia mitungi 100 hadi 200 ya gesi kwa kila chuo, ili kuendeleza kampeni ya nishati safi kwani kwa kufanya hivyo kutatoa fursa hata kwa wadau wengine wenye nia njema kuunga mkono juhudi hizo.
Aliwataka pia, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya zote kuandaa vikundi mbalimbali vitakavyowezeshwa na kugawiwa gesi kupitia halmashauri husika.
“Lake gesi ambaye ndiye mdau anayeshirikiana na serikali ameunga mkono mchakato mzima kwa kutoa mitungi 1000 ya gesi kwa mkoa mzima, lakini kuna watu hawana vikundi ndio maana bado wanaendelea na matumizi ya nishati chafu ni vyema kama halmashauri mkaunda vikundi kwa wasio navyo ili na wao wanufaike na huduma hii,”amesema.
Amesema elimu itolewe kwa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi kwa kutofautisha kati ya gesi asilia na gesi inayotoka nje ya nchi ambayo tayari imejazwa kwenye mitungi kwani jamii imekuwa ikihofia kupata madhara yatokanayo na gesi hiyo ikiwemo kulipuka na kusababisha hasara kwa binadamu.
“Mimi nitakachokifanya nitashauri na kushawishi wadau hawa wanunue mitungi kutoka lake gesi kwani tutakapoanzisha majukwaa ya nishati safi bado ataendelea kuunga mkono serikali,”ameongeza Chalamila.
Sambamba na hilo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kushiriki katika tamasha la mapishi litakalofanyika Septemba 23 mwaka huu likitarajiwa kuwa na watu 1,000 na watapata shilingi 20,000 kwa ajili ya kujaza gesi na kupika chakula kitakacholiwa na watu mbalimbali na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Mwakilishi kutoka Lake Group, Steven Mtemi amesema kama taasisi inayoshughulika na gesi wamevutiwa na jitihada za Rais Samia za kutokomeza kabisa nishati chafu kwani madhara yake ni makubwa husababisha vifo hasa kwa wanawake na kuharibu mazingira.