Collins, Sophia waitaka rekodi Olimpiki

Mchezaji wa timu ya taifa ya mchezo wa kuogelea Collins Saliboko.

WACHEZAJI wawili wana Sophia Lattif kila mmoja ameeleza shauku yake katika Michezo ya Olimpiki ni kuvunja rekodi zilizowekwa na wachezaji wengine wa Tanzania.

Saliboko amesema anatamani kupata pointi za juu na kuwashinda Khalid Rushaka na Hilal Hilal waliojitahidi mwaka 2008 na 2016.

Akizungumza na Dailynews Digital Saliboko amesema kwa uzoefu aliopata katika mashindano tofauti ya kimataifa na maandalizi mazuri ya kambi anaamini atawakilisha vizuri.

Advertisement

SOMA: TOC yataka vyama kuendesha mashindano ya Taifa

“Tangu mwaka 2017 nimekuwa nikishiriki mashindano tofauti ya kimataifa lakini Olimpiki ni mara ya kwanza, matarajio yangu ni kuvunja rekodi walizoweka wenzetu kwa kufanya vizuri zaidi,”amesema.

Kwa upande wake Sophia amesema licha ya kwamba wanapata changamoto ya kutokuwa na bwawa la mita 50 la kufanyia mazoezi atajitahidi kwa uwezo wake kulingana na mafunzo na uzoefu aliopata.

Amesema mabwawa wanayotumia mengi ni mita 25 na wanapoenda kwenye mashindano wanakuta mabwawa ya mita 50.

Mchezaji wa timu ya taifa ya Kuogelea, Sophia Lattif.

“Ni changamoto kubwa sana kufanya mazoezi kwenye bwawa la mita 25 na hapa Tanzania hakuna bwawa la mita 50, tunaenda pale Paris tutaenda kufanya mazoezi kwenye bwawa la mita 50 kabla ya kuanza kwa mashindano, naamini tutafanya vizuri,”amesema Sophia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa Chama cha Kuogelea Tanzania(TSA) Amina Mfaume amesema wamewaandaa wachezaji vizuri kiufundi na kisaikolojia kuhakikisha wanafanya vizuri.

Mmchezaji taifa ya taifa ya Kuogelea Collins Saliboko.

Michezo ya Olimpiki inatarajiwa kuanza Julai 26 na kumalizika Agosti 11 Paris, Ufaransa na kushirikisha wanamichezo mbalimbali duniani. Tanzania itawakilisha katika Riadha, Judo na Kuogelea.

Serikali imelitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha vyama vya michezo vinaleta mipango yao kwa ajili ya kujiandaa na Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2028 nchini Marekani.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Sulemani Serera ameagiza hayo katika hafla ya kuaga na kukabidhi bendera ya taifa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki Paris, Ufaransa.

Mchezaji wa timu ya taifa ya Kuogelea, Sophia Lattif.

Amesema lengo ni kuandaa timu na kuhakikisha idadi ya wachezaji inaongezeka ambao wanakidhi viwango vya kwenda kushiriki michuano hiyo mwaka 2028 kwa ajili ya kuipeperusha vema bendera ya Taifa kupitia michezo.

“Mwaka huu tunawakilishwa na wachezaji saba lengo letu ni kuona mwaka 2028 tunapeleka idadi kubwa ya wachezaji na Serikali itaendelea kushirikiana na Mashirikisho ya Michezo ili kufikia malengo yetu,” amesema Dkt Serera.