Daladala zapigwa ‘pini’ unyanyasaji wanafunzi Dar

DODOMA; WAZIRI wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa ametoa maagizo kadhaa kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA kuhakikisha yanatekelezwa ili kukabiliana na changamoto za usafiri kwa wanafunzi.
Ametoa kauli hiyo leo Februari 4, 2026 mjini Dodoma alipokuwa akizungumzia picha mjongeo ya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari, Jangwani Dar es Salaam iliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii akilalamikia kuhusu adha za usafiri kwa wanafunzi.
“Nimeona video clip kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, ambapo binti aliyejitambulisha kwa jina la Mariana Eric Mirindima ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari Jangwani akiwasilisha barua yake iliyoeleza changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanaotumia usafiri wa mabasi ya mijini, maarufu kama daladala,” amesema Waziri Mbarawa.
Amesema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhusu changamoto za wanafunzi jijini Dar es Salaam na kuzitaja baadhi kuwa ni kuanzisha huduma za mabasi maalumu yaendayo haraka kwa ajili ya wanafunzi, hususan asubuhi na jioni,.
Hatua nyingine ni kutenga mabehewa maalumu kwa ajili ya wanafunzi kwenye treni za mijini (Dar es Salaam).
“Katika kuhakikisha utekelezaji mzuri wa hatua hizi, pamoja na kujibu changamoto zilizowasilishwa na mwanafunzi Mariana, ninaiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutekeleza yafuatayo:
“Kuhakikisha zoezi la kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu (makondakta) kwenye mabasi linafanywa kwa kasi katika miji yote nchini, na kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria kwa madereva na makondakta watakaobainika kuwanyanyasa wanafunzi;
“Kuimarisha udhibiti wa nauli maalumu za wanafunzi, staha ya huduma na usalama wao kwa wakati wote;
“Kuhakikisha treni za abiria, daladala zote nchini pamoja na mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani zimeandikwa namba za bure ili abiria waweze kupiga LATRA 0800 11 00 19 na 0800 11 00 20; na
“Kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza kwenye vituo vya daladala hasa nyakati za asubuhi na jioni kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri,” amesema Waziri Mbarawa.

