TIMU ya kuogelea ya Dar es Salaam imepania kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika Kenya Februari 15 na 16.
Akizungumza na Daily News Digital Kocha wa timu hiyo Kanisi Mabena amesema kwa maandalizi mazuri waliyofanya anaamini watafanya vizuri.
“Mashindano haya ni muhimu kwetu kwenda kuongeza uzoefu, kikosi changu kimejipanga kwa muda mrefu naamini kitafanya vizuri,”amesema.
Amesema hana hofu kwasababu wachezaji wengi alionao wana uzoefu na mashindano mbalimbali wanachoenda kufanya ni kuendelea kupambana na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Kikosi cha wachezaji sita kiliondoka Dar es Salaam Februari 13 kuelekea Kenya tayari kupambana na kurudi na medali za ushindi.
Mbali na Dar Swim, timu nyingine za Tanzania zitakazoshiriki ni Reptide ya Arusha na Tanzania Swim Squad yenye wachezaji kutoka klabu tofauti.