DC Iramba: Tutapeleka maji vijiji vilivyosalia

MKUU wa Wilaya ya Iramba mkoani, Singida Suleiman Mwenda amewahakikishia wananchi wa Tarafa ya Shelui hususani wakazi wa vijiji vya kata za Mtoa, Shelui na Mgongo ahadi ya Rais itakelezwa kwa kuhakikisha vijiji vyote 12 vilivyosalia vinapata maji kutoka Ziwa Victoria wa Tinde – Shelui.

Akijibu maswali ya wanakijiji wa vijiji vya Mseko, Kizonzo, Kinkungu, Mtoa na Kinkungu katika ziara ya kusikiliza kero za wananchi hao, DC Mwenda amewahakikishia wananchi wa vijiji hivyo kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho kutekeleza ahadi aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa wananchi alipofanya mkutano wa hadhara Shelui.

Advertisement

Katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan wilayani Iramba Oktoba 17,2023 alizindua mradi wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Tinde – Igunga hadi Shelui wenye gharama ya Sh bilioni 24.6 na wananchi zaidi ya 40,000 wa vijiji vya Tinde mkoani Shinyanga na Shelui mkoani Singida tayari wanapata huduma ya majisafi na salama, na kutekeleza awamu ya pili utagharimu Sh bilioni 16.2.

Aidha DC Mwenda amesema kuwa mara baada ya uzinduzi wa mradi huo wanufaika wa mradi huu ni vijiji viwili ambavyo ni Shelui na Mgela, maagizo ya Rais kwa Wizara ya Maji ni kuhakikisha mradi huo unawafikia wananchi wa vijiji 12 vilivyobaki vya kata za Mgongo, Shelui Mtoa na Ntwike.

“Waziri wetu wa maji ni kiongozi msikivu na mchapa kazi na Kila tunapopata changamoto anatatua kwa haraka. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Mji wa Kiomboi (KIUWASA) alifika kwangu akiwa na changamoto, tulikwenda Dodoma kumuona Mhe. Waziri wa Maji na ndani ya miezi 2 changamoto zote zilitatuliwa ikiwemo mamlaka hiyo ya maji ikapatiwa gari jipya toka wizarani, suala la kutekeleza ahadi hii ya Rais nina imani kubwa tutalikamilisha mapema mwakani kwa kushirikiana na watu wa RUWASA na Wizara ya Maji,” alisisitiza DC Mwenda.