Demokrasia si lazima upinzani ushinde, chama tawala kishindwe

NIANZE makala yangu kwa kusema kuwa,ipo tofauti moja tu katika uwanja wa demokrasia ukilinganisha na uwanja wa soka.
Katika uwanja wa soka timu zinapoingia uwanjani mbali na fainali au mazingira maalumu yanayohitaji bingwa apatikane na hivyo kuweka kipindi cha kuanzia penati tano kila upande, wachezaji na mashabiki hutegemea jambo moja kati ya matatu litokee, yaani ama timu ifunge, ifungwe ama zitoke suluhu yaani bila kufungana.
Katika siasa mambo ni tofauti; ni ama ‘ndiyo’ au ‘hapana’ yaani kupata au kukosa ushindi. Katika masuala ya siasa na demokrasia jibu ni moja, kuchaguliwa ama kutochaguliwa; kushindwa au kushinda katika uchaguzi na hapo, asiyekubali kushindwa si mshindani katika uwanja wa demokrasia.
Ikitokea kura zikalingana kati ya vyama vyenye ushindani wa juu, hapo ndipo uchaguzi hufanyika katika duru nyingine ili kupata mshindi. Katika uchaguzi wa kisiasa na demokrasia uchaguzi ni lazima upinzani ushinde, au ushindwe na ama chama tawala kishinde au kishindwe tujue moja.
Katika soka, nashukuru kwamba hakuna ugonjwa wa kwamba ili mchezo uonekane umechezwa kwa haki eti lazima timu ‘A’ ishinde dhidi ya timu ‘B’ au eti lazima timu B ishinde dhidi ya timu A. Ndivyo ilivyo hata katika siasa na demokrasia ya vyama vingi nchini.

Vyama vya upinzani na hata chama tawala (Chama Cha Mapinduzi – CCM) vinapoingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wowote ama uwe mdogo, uchaguzi wa serikali za mitaa au uchaguzi mkuu, lazima vijindae kwa jawabu moja watakalotoa wananchi ama kukichagua, au utokukichagua.
Katu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisikengeuke na kudhani ili demokrasia ionekane, lazima kishinde maana kudhani hivyo, ni kujaribu ‘kubemenda’ demokrasia ya vyama vingi nchini.
Kadhalika, vyama vya upinzani kasumba ya ‘kulisha wafuasi wao sumu’ kwamba licha ya umri wao mdogo ukilinganisha na CCM na licha ya kuwa hawajawahi kuongoza nchi na kwamba wananchi hawajaviamini kushika dola, visiwalishe wafuasi ‘matangopori’ kuwa ili demokrasia itendeke na ionekane imetendeka, lazima chama tawala kishindwe. Huo ni uongo na ni kubemenda demokrasia nchini.
Ni sawa na baadhi ya watu wanaokengeuka na kusifia wahuni katika baadhi ya nchi wanaofanya uporaji kwa kujificha katika maandamano kwamba hao ndio wanaojua na kuishi demokrasia. Huo ni uongo, ni sumu isiyopaswa kujaribiwa ana kwa kuilamba au kufanya vurugu kwa lengo la kuabudu uhuru usio na mipaka.
Ni uhalifu na katu si kustawi kwa demokrasia maana demokrasia si uhuni au kukataa haki za wengine. Ndio maana katika moja ya ziara zake wilayani Temeke, Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla anawataka Watanzania kuogopa ‘sumu’ kwamba chama tawala kikishindwa, ndipo demokrasia itakuwa imetamalaki.

Kwangu, kasumba hiyo ni ugonjwa mbaya usiopaswa kupewa nafasi wala kurithishwa kwa vizazi vijavyo vya siasa kwa kuwa ugonjwa huo unaweza ukalisukuma taifa kuingia katika ‘mdomo wa mamba wenye meno makali ya kutafuna na kumeza amani ya nchi.’
Ndio maana ni muhimu vyama hasa vya upinzani kujiuliza kuwa, kama demokrasia ni kushindwa kwa chama kilichopo madarakani wakati wa uchaguzi, siku vikishika madaraka navyo havitapaswa kushinda tena ili demokrasia ionekane imetendeka?
Kimsingi, kufikiri hivyo ni dalili za kukomaa kwa msongo wa mawazo ya kisiasa kunakoelekea kuwa tatizo la afya ya akili kwa vyama vyenye ugonjwa wa kudhani hivyo.
Kinachoshangaza na kuibua maswali ni kuwa, je siku ikitokea mathalani chama kinachoonesha imani ndogo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kikatangazwa ushindi, kitatangaza kwamba tume imetenda haki au kitasema kwa ushindi wake tume haijatenda haki na kukataa ushindi.
Ndio maana Makalla ananukuliwa akisema, “Kwa tume hii ilivyo huru itatenda haki na sisi (Watanzania) tunataka itende haki maana kuna tabia imejengwa kwamba chama tawala kinaposhindwa ndiyo demokrasia ya kweli, akubali pia chama kinaposhinda ni demokrasia ya kweli.”

Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuph Makamba alipenda kusema, “Ajisifu atokaye vitani si aendaye maana atokaye, ana kitu cha kuonesha.”
Ndivyo ilivyo kwamba, tofauti na chama tawala ambacho kina vitu vingi ambavyo ni ushahidi wa utawala bora na maendeleo, vyama vya upinzani bado vina kazi ya kujinadi na kujitangaza zaidi kwa wananchi kuwa vikiingia madarakani vitaimarisha tunu ya amani, umoja na mshikamano.
Kwamba, vitakuwa vyama vinavyopigania maendeleo na ustawi wa watu kupitia siasa safi na uongozi bora. Vijue kuwa, kama bado watu wana shaka katika maeneo hayo yani amani na maendeleo kutokana na ‘ugeni’, wanaweza kusita kuviweka madarakani hadi ‘macho yatakapoona na akili zao kuamini’ kuwa vyama vinaendesha siasa safi na uongozi bora usio na dalili za kuabudu vurugu, bali kuchochea maendeleo na amani ya watu.
Katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025, vyama vya upinzani vinapaswa kuonesha Watanzania kwamba, vimekomaa na tayari vimepata uzoefu kwa kuona chama tawala kinavyofanya.
Vyama vyote viendeshe kampeni za kistaarabu vikizingatia ratiba na kuepuka matusi dhidi ya washindani na pia, vioneshe njia ya kuelekea maendeleo halisi ya Watanzania sambamba na ukomavu wa kukataa aina zozote za vurugu na kususa maana asiyekubali kushindwa, si mshindani.
Vyama viandae ilani nzuri zitakazovutia wapigakura huku vikizingaiti na kuonesha namna ilani hizo zitakavyotekelezeka ili zisiwe ‘maji ya moto yasiyounguza nyumba.’
Ili vioneshe hayo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inaviagiza vyama vya siasa kuimarisha uongozi wa kidemokrasia, haki na uwajibikaji hata kupitia uteuzi wa wagombea huku vikifanya kampeni safi na kushiriki uchaguzi kwa njia halali kwa kuepuka uhalifu ukiwamo wa matumizi ya rushwa katika uchaguzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila anasema hayo mwishoni mwa Aprili mwaka huu wakati akifungua warsha kwa viongozi wa vyama vya siasa kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Katika warsha hiyo, Chalamila anasema viongozi wa vyama kama taa za vyama vya siasa wana wajibu mkubwa kuhakikisha vinazingatia kanuni na maadili ya uchaguzi kwa kuwabaini, kuchunguza na kuwaondoa wote wanaohusika na vitendo vya rushwa na uvunjifu wa amani.
Kimsingi, jukumu la kukataa wagombea, wanasiasa na vyama vinavyotumia nguvu kubwa kunadi uvunjifu wa amani linasemwa na wadau mbalimbali kuwa, si tu la vyombo vya dola, bali hasa la wananchi wote na hasa wapigakura kupitia sanduku la kura.
Ndio maana kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 kila mmoja azingatie kuwa, demokrasia si lazima upinzani ushinde na chama tawala kishindwe au eti kuacha watu wajifanyie watakavyo.
Good post. I’m dealing with a few of these issues as well..
penis enlargement