Dk. Mwigulu aomba nyongeza ya bajeti shilingi bil 945.7

DODOMA: WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amewasilisha bungeni pendekezo la kuomba nyongeza ya bajeti ya serikali ya mwaka 2024/2025 yenye jumla ya Shilingi bilioni 945.7.

Akiwasilisha pendekezo hilo bungeni mjini Dodoma, Dk. Mwigulu alisema kuwa kwa mujibu wa ibara ya 137(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifungu cha 43, sura ya 439, serikali ina jukumu la kuwasilisha bungeni pendekezo la kuomba ridhaa ya Bunge ya kupatiwa nyongeza ya bajeti ya serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inazidi kuimarika.

Alisema kuwa nyongeza hii ya bajeti inalenga kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta muhimu ikiwemo elimu, afya, taasisi za utalii, na pia kutoa ufadhili kwa programu za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Advertisement

Dk. Mwigulu alifafanua kuwa mgawanyo wa fedha hizo utazingatia maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, hasa katika kuimarisha nguvu kazi yenye ujuzi kwa kuhakikisha utekelezaji wa mitaala mipya ya elimu ya awali. SOMA: Akiba fedha za kigeni dola mil. 5,345.5

“Mgawanyo wa fedha hizi utazingatia mapendekezo ya sekta tajwa, makubaliano ya serikali na washirika wa maendeleo pamoja na ushauri wa kamati ya kudumu ya bunge. Hii ni ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mipango unazingatia mahitaji halisi ya wananchi na nchi yetu,” alisema Dk. Mwigulu.

Pia, alieleza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa programu za maendeleo ili kufikia malengo ya kitaifa ya kujenga uchumi imara na unaozingatia ustawi wa jamii.

Dk. Mwigulu alisisitiza kuwa nyongeza hii ya bajeti inaimarisha uwezo wa serikali katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinatumika kwa ufanisi katika sekta zote muhimu.

Katika kumalizia, Dk. Mwigulu alisisitiza kuwa mpango huu ni sehemu ya juhudi za serikali katika kufikia malengo ya kuimarisha huduma za jamii na kuboresha mazingira ya kiuchumi na kijamii, huku akiahidi kuwa usimamizi wa fedha hizo utafanyika kwa uwazi na kuzingatia vipaumbele vya taifa.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *