Mwinyi: Hakuna atakayedhulumiwa fidia

MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuunda Tume Maalum itakayofanya tathmini ya kina kuhusu fidia walizolipwa wananchi waliopisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo ya Fumba, Nyamanzi, Dimani na Bweleo, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake stahiki.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo, Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi jana, Dk. Mwinyi alisema tume hiyo itapitia na kuhakiki fidia zote zilizolipwa kwa wananchi kwa lengo la kujiridhisha kuwa kila anayestahiki amelipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Alisema serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na udanganyifu katika michakato ya fidia, ikiwemo wale wanaojenga au kuotesha miti kwa haraka katika maeneo yaliyopangwa kwa miradi ya maendeleo kwa nia ya kudai fidia isiyostahili. “Serikali haitaridhia mtu yeyote kudhulumiwa. Kila anayestahiki atalipwa kwa mujibu wa eneo analomiliki. Lengo letu ni kuwaondoa wananchi katika umasikini, si kuwaingiza katika umasikini,” alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, aliagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu kabla ya kutekelezwa kwa miradi yoyote ya maendeleo, sambamba na kupiga picha za maeneo husika ili kuweka kumbukumbu sahihi zitakazosaidia kuepusha migogoro ya ardhi.

Dk. Mwinyi aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kudhibiti vitendo vya udanganyifu na wizi wa ardhi, akisisitiza kuwa miradi ya maendeleo inalenga kuboresha maisha ya wananchi, si kuwadhuru. SOMA: SMZ kujenga hospitali mbili za rufaa

Katika mkutano huo, aliomba wananchi kumpa ridhaa ya kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa awamu nyingine, ili aweze kukamilisha utekelezaji wa ahadi zake na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Muhammed Said Dimwa, alisema chama hakikukosea kumteua Dk. Mwinyi kugombea urais wa Zanzibar, akimwelezea kama kiongozi mzalendo, mtekelezaji wa ahadi na mwenye dira ya maendeleo ya kweli kwa taifa.

Baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kutoa maoni yao walimshukuru Dk. Mwinyi kwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi alizozitoa awali, hatua waliyosema imesaidia kupunguza changamoto nyingi za kijamii katika maeneo yao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button