TANZANIA inatarajia kunufaika na miradi ya nishati jadidifu yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 18 kutokana na kuundwa kwa Sekretariati ya Programu ya Afrika kuhusu Nishati safi ya Kupikia kwa wanawake ambayo inaweza kutengeza ajira nchini.
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Christina Mndeme amesema hayo leo Oktoba 23, wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha wataalam cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan.
SOMA; Serikali yaja na mkakati nishati safi ya kupikia
Amesema miradi inayotarajiwa kuinufaisha Tanzania itafadhiliwa na Benki ya Dunia, Taasisi ya Afrika 50 na Shirika la Nishati la Afrika kwa kushirikiana na kampuni ya China Renewable Energies.
Pia, amesema Dola za Marekani milioni moja zimeahidiwa na Serikali ya Norway pamoja na International Renewable Energy Agency (IRENA) pamoja na kuendelea kuisaidia Tanzania katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, hususan utekelezaji wa Mchango wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC).
Mndeme amesema kuwa hatua hiyo inatokana na maafanikio yaliyopatikana wakati wa Mkutano wa 28 (COP28) uliofanyika kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 Dubai, Jamhuri ya Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 28 kupitia maonesho umesaidia kuitangaza Tanzania kimataifa katika nyanja za hifadhi ya mazingira na mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kikao kazi hicho chenye lengo la kujadiliana na kutoa mapendekezo kuhusu maandalizi ya COP 29, kimeshirikisha wajumbe zaidi ya 60 kutoka Wizara, Idara za Serikali na Taasisi, Wadau wa Maendeleo, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia (AZAKI) za Tanzania Bara na Zanzibar.