WAKUU wa hifadhi nchini wametakiwa kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi kwa lengo la kuendeleza sekta ya maliasili na utalii na kuimarisha mahusiano mazuri baina yao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana agizo hilo alipozungumza na wahifadhi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii likiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI) jana.
SOMA: Wizara ya utalii yadhibiti wanyamapori wakali
Katika kikao hicho, Waziri Chana amesema: “Wakuu wa hifadhi muonane na wanakijiji muongee nao ili muwape elimu ya uhifadhi na muwashauri wawe na maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) kwenye mapori yetu ya TAWA, TANAPA na TFS,” Dk Chana amesema.
Aidha, amewataka wahifadhi hao kuhakikisha wanaweka alama zinazoonekana katika hifadhi ili kuimarisha mipaka kwa kushirikisha serikali za vijiji vinavyozunguka maeneo hayo.