WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana amesema wizara imeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kudhibiti changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu huku akisisitiza mkakati wa kuongeza ndege nyuki ili kudhibiti tembo.
Waziri Chana ametoa kauli hiyo leo Oktoba 3,2024 wakati akizungumza na watumishi wa Hifadhi ya Taifa Katavi, Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi.
“Mhe. Rais tayari ametuelekeza kudhibiti wanyama wakali ikiwemo tembo hivyo tunahamasisha vijana katika vijiji vilivyoko pembezoni mwa maeneo ya hifadhi kujitokeza kujiandikisha kupata mafunzo ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika Chuo cha Likuyu Sekamaganga kilichopo Namtumbo mkoani Ruvuma,”amesisitiza Chana.
SOMA: Dk Chana akagua chanzo cha maji Miti Mbizi
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kujenga vituo vya askari kuhakikisha kuna uhifadhi endelevu na kudhibiti wanyamapori wakali.
Chana ameelekeza kwenye vituo vya askari vilivyojengwa Wilaya ya Kalambo na Mbarali vikamilike kwa wakati na viwe na rasilimali watu ili vifanye kazi iliyokusudiwa.
SOMA: Dk Chana: Ajenda uhifadhi mazingira zidumu
Aidha, amesema wizara inaendelea na maboresho mbalimbali ya kutangaza vivutio vya utalii.
“Tayari tuna maelekezo ya Mhe Rais kuendelea kuongeza mapato kutokana na utalii na tunachangia asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za nje takribani Dola bilioni 3.6,” Dk Chana amesema.
Katika hatua nyingine amewapongeza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchi nzima kwa kazi nzuri ya uhifadhi wanayoifanya huku akisisitiza vijiji kuweka ajenda ya kudhibiti moto, kutunza misitu na mazingira iwe ya kudumu.