LUSAKA, ZAMBIA: Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Bodi ya Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kimiundombinu ili kuboresha huduma za nishati katika nchi zao.
Wakati wa kikao baina ya Bodi hizo, zilizokutana Jumatatu, Ofisi za ERB Lusaka, imebainishwa kuwa hivi karibuni taasisi hizo za usimamizi zitasaini hati ya makubaliano kwa ajili ya ushirikiano huo.
Baadhi ya maeneo ambayo EWURA na ERB watashirikiana ni pamoja na kubadilishana taarifa za kitaalamu, kiuchumi na kimiundombinu, kujengea uwezo wataalamu, na kubadilishana uzoefu katika masuala ya kitaalamu.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof Mark Mwandosya, alisema kuwa ushirikiano kati ya EWURA na ERB tayari umeleta mafanikio makubwa katika udhibiti wa sekta za petroli, gesi asilia, na umeme.
Prof Mwandosya aliongeza kuwa ushirikiano huo umechangia kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya usalama, mifumo ya kisheria, na ufanisi katika uendeshaji wa sekta hizo.
“Moja ya mafanikio makubwa ya ushirikiano wetu ni juhudi za pamoja katika ukaguzi wa bomba la mafuta la TAZAMA. Ukaguzi huu haujaimarisha tu usalama na ufanisi wa miundombinu hii muhimu, bali pia unadhihirisha dhamira yetu ya kuendeleza ubora wa udhibiti katika ukanda huu,”
alisema Prof Mwandosya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, James Banda alisema kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya sekta wanazosimamia na kusisitiza kuwa kusainiwa kwa hati ya makubaliano kutatoa msukumo zaidi katika kuboresha huduma za nishati na kuimarisha ufanisi wa kiutendaji.
Kabla ya pande hizo kukutana, mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Prof Mark Mwandosya ameongoza wajumbe wa bodi hiyo na menejimenti kukagua Bomba la Mafuta la TAZAMA linaloanzia Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola, Zambia kwa lengo la kufahamu changamoto za kiuendeshaji na kuzitafutia ufumbuzi.
SOMA:
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyoanza Machi 21, 2025, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati ya Bodi ya EWURA, Ngosi Mwihava alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua uendeshaji wa bomba la TAZAMA na masuala yote ya kiuchumi na kimiundombinu.
“Moja ya jukumu la EWURA katika sekta ya petroli ni kudhibiti miundombinu inayohusu ya usafirishaji wa mafuta na gesi asilia, hivyo ziara hii ni mahususi kwa ajili ya kukagua bomba, kuona changamoto zilizopo na kuangalia namna tunavyoweza kusaidia utatuzi wa changamoto hizo ili kuendelea kuboresha huduma za usafirishaji wa mafuta kupitia bomba hili,” Mwihava alisema.
Mwihava aliongeza pia kuwa ziara hiyo ni fursa ya Bodi ya EWURA na ya Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya upangaji wa bei, mikakati ya uhifadhi wa mafuta ya akiba na kujengea wataalamu uwezo
Ujumbe huo umetembelea kituo cha Chilolwa cha kuangalia usalama wa bomba la mafuta, kituo cha kusukuma mafuta kilichopo Chinsali na ghala la kuhifadhia mafuta lililopo Mpika.