FDA yaidhinisha kidonge Wegovy kupunguza uzito

MAMLAKA ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) imeidhinisha matumizi ya toleo la vidonge vya dawa ya kupunguza uzito ya Wegovy, hatua inayofungua ukurasa mpya katika matibabu ya unene kupita kiasi.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni ya dawa ya Novo Nordisk ya Denmark, idhini hiyo inaifanya Wegovy kuwa dawa ya kwanza ya kupunguza uzito katika mfumo wa kidonge kupata kibali cha FDA. Novo Nordisk imesema kidonge hicho kinachotumiwa mara moja kwa siku ni rahisi zaidi kwa wagonjwa ikilinganishwa na sindano, huku kikiwa na ufanisi unaolingana na toleo la sindano lililokuwapo awali.
Idhini hiyo inafuatia matumizi ya awali ya Wegovy kwa njia ya sindano baada ya FDA kuiruhusu kwa ajili ya kupunguza uzito. Katika majaribio ya kitabibu yaliyofanywa na kampuni hiyo, kidonge cha Wegovy kimeonyesha uwezo wa kupunguza uzito kwa wastani wa asilimia 16.6. SOMA: Mwenye kilo 145 afanyiwa upasuaji kupunguza uzito
Aidha, takribani theluthi moja ya washiriki wapatao 1,300 walioshiriki katika majaribio hayo walipunguza uzito kwa asilimia 20 au zaidi. Hadi sasa, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limesema limewasiliana na FDA kwa ajili ya kupata maelezo zaidi kuhusu idhini hiyo. Kidonge cha Wegovy kinatarajiwa kuanza kupatikana rasmi nchini Marekani mapema Januari 2026.



