GGML yafadhili makazi ya polisi Mgusu – Geita

GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imekamilisha ujenzi wa nyumba mbili (nyumba pacha) za askari wa polisi katika mtaa wa Mgusu kata ya Mgusu wilayani Geita mkoani hapa.
Ufadhili huo umegharimu kiasi cha sh milioni 77 ambazo zimezotumika kukamilisha maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi lengo ili kuboresha makazi ya askari polisi.
Kaimu Mkurugenzi wa GGML, Duan Campbell ametoa taarifa hiyo katika hafla ya kukabidhi nyumba hizo kwa jeshi la polisi akieleza mradi ulianza Januari 2023 kuunga mkono ustawi wa askari.

Duan amesema kukamilika kwa mradi huo ni muhimu kwani siyo tu unajenga mahusiano ya mgodi na jamii lakini pia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yanayozunguka mgodi.
Amesema sera ya GGML inaamini kuwa Jamii imara inategemea taasisi imara za ndani, na moja ya taasisi zinazoshikilia uimara na ustawi wa jamii kila siku ni jeshi la polisi.

“Askari polisi wanaposaidiwa kwa kupata makazi bora, utulivu na heshima, uwezo wao wa kuitumikia jamii unaimarika zaidi, hali hii huongeza utayari wa kazi, huimarisha molari.
“Kampuni ya GGML tunaamini kwamba Geita salama na yenye ulinzi wa uhakika inachangia moja kwa moja uendelevu wa shughuli zetu”, amesema na kuongeza;

“Usalama hauishii ndani ya mgodi pekee, bali usalama upo pia majumbani, barabarani, shuleni, na mitaani ambako watu wanaishi na kufanya kazi”, amesisitiza Duan.
Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mgusu, Nazoro Marcel amesema mradi ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2019/20 kupitia nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo kwa kuchangia madini ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa msingi na boma yaliyogharimu sh milioni 19.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema ushirikiano kati ya wananchi, wadau wa maendeleo na viongozi wa serikali imeleta matokeo chanya kupunguza matukio ya uharifu Geita.
Kamanda Jongo amekiri kuwa mchango wa GGML kwenye sekta ya ulinzi na usalama unawafanya kuwa wadau wakubwa wa amani ambapo wamesaidia kuboresha utendaji wa polisi mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameipongeza GGML kwa msaada huo huku akiwaomba kutenga bajeti ya ujenzi wa kituo bora cha polisi cha kata ya Mgusui li kukidhi mahitaji ya eneo hilo.



